Manchester, England
Kiungo wa Man City, Kevin de Bruyne atakuwa nje ya uwanja kwa takriban miezi minne wakati klabu yake ikiangalia kama atahitaji kufanyiwa upasuaji wa matatizo ya misuli yanayomkabili.
De Bruyne aliumia Ijumaa iliyopita na kutoka nje ya uwanja huku akichechemea katika dakika ya 23 wakati Man City ikiumana na Burnley katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England (EPL) msimu wa 2023-24.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 32, pia aliumia na kutoka nje ya uwanja Juni mwaka huu katika mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Inter Milan, mechi ambayo Man City iliibuka na ushindi na kubeba taji hilo.
De Bruyne ambaye pia ni kiungo wa timu ya Taifa ya Ubelgiji, alizikosa mechi zote za Man City za maandalizi ya msimu wa 2023-24 kabla ya kurudi uwanjani kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Arsenal ambayo aliingia kipindi cha pili, mechi ambayo Man City ilishindwa kutamba.
“Ni maumivu makubwa, tunawajibika kuamua kama atahitaji kufanyiwa upasuaji au la, lakini atakuwa nje ya uwanja kwa miezi michache,” alisema kocha wa Man City, Pep Guardiola.
Pep ambaye pia alifafanua kwamba mchezaji huyo anasumbuliwa na tatizo lile lile la misuli, uamuzi wa kumfanyia upasuaji utajulikana siku chache zijazo ingawa aliweka wazi kuwa kwa hali ilivyo sasa, De Bruyne atakosekana uwanjani kwa miezi mitatu au minne.
Katika hatua nyingine, Pep pia alisema kwamba De Bruyne aliwahi kuwaambia mapema mwezi huu kwamba katika miezi miwili iliyopita alikuwa akicheza huku akiwa mwenye maumivu ya misuli ingawa kabla ya mechi na Burnley walichukua tahadhari zote.
“Ninachoweza kusema ni kwamba kuumia kwa Kevin ni pigo kwetu, tumepoteza kitu kikubwa, Kevin ana kiwango cha kipekee ambacho unaweza kukikosa kwa mechi moja au mbili lakini si kwa kipindi kirefu, hakika ni jambo gumu kwetu, ingawa pia tunatakiwa kuangalia mbele, tuna suluhisho japo mbinu na uwezo wa Kevin ni mambo yasiyo na mbadala,” alisema Pep.
Katika msimu uliopita wa 2022-23, ambao Man City ilibeba mataji matatu ya FA, EPL na Ligi ya Mabingwa Ulaya, De Bruyne aliifungia timu hiyo mabao 10 na kutoa asisti 31.