Buenos Aires, Argentina
Beki wa zamani wa Brazil, Marcelo ambaye kwa sasa anaichezea Fluminense ya Brazil, amefungiwa mechi tatu baada ya kumvunja mguu beki Luciano Sanchez wa Argentinos Juniors katika mechi ya Copa Libertadores wiki iliyopita.
Mbali na kufungiwa mechi tatu, Marcelo, 35, (pichani), ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa Real Madrid, ametozwa faini ya Dola 6,000 na Shirikisho la Soka Marekani Kusini au CONMEBOL.
Katika tukio hilo, Marcelo alikuwa akiuwahi mpira kwenye miguu ya Sanchez lakini mguu wake wa kushoto ulikwenda moja kwa moja hadi kwenye mguu wa mchezaji huyo na kumuumiza vibaya.
Baada ya tukio hilo, Sanchez alibaki chini akiugulia maumivu kabla ya kutolewa akiwa amebebwa kwenye machela na baadaye kuelezwa kwamba amevunjika mguu huku daktari wa timu hiyo akisema kwamba hajawahi kuona tukio kama hilo hapo kabla.
Marcelo baada ya kufanya kosa hilo alitolewa na wakati akitoka uwanjani alionekana mwenye huzuni na baadaye kupitia mtandao wa Instagram alitoa kauli akionekana mwenye kujutia kilichotokea.
“Nimejikuta katika tukio gumu mno uwanjani, nimemuumiza mchezaji mwenzangu bila kukusudia, namuombea apone haraka iwezekanavyo,” alisema Marcelo.
Mechi hiyo ya kwanza ya hatua ya 16 bora ya Copa Libertadores iliisha kwa sare ya bao 1-1 na Fluminense tayari imemkosa Marcelo katika mechi ya marudiano ambayo timu hiyo ilishinda kwa mabao 2-0 na sasa inasubiri kumkosa katika mechi nyingine mbili.