Na mwandishi wetu, Tanga
Simba leo Jumapili imeuanza vyema msimu wa 2023-24 kwa kuibwaga Yanga kwa penalti 3-1 kwenye Uwanja wa Mkwakwani na kubeba Ngao ya Jamii huku kipa wake, Ally Salim kwa mara nyingine akiibuka shujaa wa penalti.
Hii inakuwa mara ya pili kwa Ally Salim katika siku za karibuni kuibeba Simba kwenye penalti, baada ya kufanya hivyo katika mechi ya kwanza Alhamisi iliyopita dhidi ya Singida Fountain Gate alipookoa penalti na kuifanya Simba ifuzu hatua ya fainali kwa ushindi wa penalti 4-2.
Katika mechi ya leo, timu hizo zilipambana kwa dakika 90 za kawaida lakini hadi mwamuzi anapuliza filimbi ya kumaliza mchezo, hakuna timu iliyoliona lango la mwenzake.
Kwa ushindi huo Simba wametawazwa rasmi kuwa mabingwa wapya wa michuano hiyo inayoashiria kuanza kwa Ligi Kuu NBC msimu mpya wa 2023-24 na wanalichukua taji hilo kutoka mikononi mwa mahasimu wao Yanga waliolibeba msimu uliopita.
Penalti za ushindi za Simba zilifungwa na Muzamiru Yassin, Willy Onana na Jean Baleke aliyepiga penalti ya mwisho iliyoihakikishia Simba ushindi wakati waliokosa ni Saido Ntibazonkiza na Moses Phiri aliyepaisha.
Kwa upande wa Yanga aliyefunga penalti ni Aziz Ki peke yake na waliokosa ni Pacome Zouzoua, Khalid Aucho na Yao.
Katika dakika 90 za kawaida kila timu ilipambana kusaka bao, Simba walifanya shambulizi katika dakika ya 23, Zimbwe alimuunganishia pasi Luis Miquissone lakini mchezaji huyo alijichanganya wakati akiupiga mpira na kuokolewa na mabeki wa Yanga.

Dakika tano baadaye, Simba walifanya shambulizi jingine lililotokana na pasi ya Clatous Chama kwa Kanoute na Kanoute kumrudishia tena Chama lakini shuti la Chama lilitua mikononi mwa kipa Djugui Diarra wa Yanga.
Dakika ya 31 Yanga nao walifanya shambulizi baada ya Musonda kupiga krosi ambayo kipa Ally Salim aliokoa lakini Clement Mzize akiwa karibu na eneo hilo alishindwa kuipatia bao Yanga.
Dakika nane baadaye Yanga walifanya tena shambulizi baada ya Maxi Nzengeli kupiga krosi ndefu iliyomfikia Mzize lakini shuti lake liliokolewa na kipa Ally Salim.
Timu hizo zilifanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji ikiwamoYanga kumtoa Mudathir Yahya na kumpa nafasi Jonas Mkude kucheza kwa mara ya kwanza dhidi ya Simba, timu aliyoichezea kwa miaka mingi.