London, England
Arsenal hatimaye imemsajili kiungo Declan Rice kutoka West Ham kwa ada ya Pauni 100 milioni ikiibwaga Man City ambayo pia ilikuwa ikimtaka mchezaji huyo.
Rice mwenye umri wa miaka 24 amesaini mkataba wa miaka mitano na Arsenal huku kukiwa na kipengele kinachompa nafasi ya kuongeza mwaka mwingine mmoja.
Katika siku za karibuni, klabu za Arsenal na Man City zilikuwa vitani katika kuisaka saini ya Rice ambaye hata hivyo iliwahi kuelezwa kwamba mwenyewe anaitamani zaidi Arsenal kuliko Man City
“Nimekuwa nikiiangalia Arsenal kwa misimu kadhaa iliyopita, ni timu yenye malengo inayoendelea nayo,” alisema Rice.
“Si msimu uliopta tu bali hata msimu kabla ya huu, walimaliza nafasi ya tano lakini unaweza kuona aina yao ya uchezaji aliyokuwa akiifanyia kazi Mikel (Arteta),” aliongeza Rice.
“Msimu uliopita ulikuwa wa kipekee waliibwaga karibu kila timu kwenye maji isipokuwa Manchester City,” aliongeza Rice.
Rice amekuwa kivutio katika timu ya West Ham chini ya kocha David Moyes lakini umaarufu wake ulikuwa juu zaidi akiwa na timu ya England kwenye fainali za Kombe la Dunia, akazidi kuzungumzwa alipoiwezesha West Ham kubeba taji la Europa Conference Ligi.
Usajili wa Rice ni wa tatu katika kikosi cha Arsenal, timu ambayo imedhamiria kuwa bora zaidi baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu England (EPL) msimu uliopita wa 2022-23.

Arsenal tayari imekamilisha usajili wa Mjerumani Kai Havert kutoka Chelsea kwa ada ya Pauni 65 milioni pamoja na beki Mholanzi, Jurrien Timber kutoka Ajax kwa ada inayotajwa kufikia Pauni 38.5 milioni.
Akimzungumzia Rice, kocha wa Arsenal, Mikel Arteta alisema kwamba hakuna ubishi kwamba ataingiza kiwango bora katika timu na ana kipaji kikubwa ambacho kitampa nafasi ya kupata mafanikio akiwa Arsenal.
“Declan ana uzoefu katika Ligi Kuu England akiwa ndio kwanza ana miaka 24, amekuwa nahodha wa klabu nzuri ya West Ham kama ambavyo wengi tumemshuhudia na hivi karibuni amebeba taji la Ulaya,” alisema Arteta.
Arsenal imefanikiwa kuinasa saini ya Rice baada ya ofa zao mbili kukataliwa wakati Man City wao ofa yao moja ya Pauni 90 milioni ilikataliwa.
Rice ameifungia West Ham mabao 15 katika mechi 245, alijiunga na akademi ya timu hiyo akiwa na miaka 14 baada ya kuachwa kwenye akademi ya Chelsea.
Alisaini mkataba na kikosi cha kwanza cha West Ham, Desemba 2015 na kuanza kuiwakilisha timu hiyo kwenye EPL msimu wa 2016-17 akiingia kutokea benchi kwenye mechi na Burnley kabla ya kuanza kipindi cha kwanza mara ya kwanza msimu huo huo katika mechi na Southampton.

Rice alikabidhiwa unahodha West Ham mwaka jana baada ya Mark Noble kustaafu na ingawa huo ulikuwa msimu wake wa mwisho, Rice amemaliza vizuri kwa kubeba taji la Europa Conference na kufuta ukame wa miaka 43 wa timu hiyo bila taji lolote kubwa.
“Katika soka fursa kubwa hujitokeza, klabu kubwa kama Arsenal imekuja kwangu na kwa hakika ni vigumu kuikataa, nayaangalia yajayo ya Arsenal kutokana na aina ya kikosi ambacho Mikel anakitengeneza, nina furaha kubwa kufanya kazi na Mikel,” alisema Rice.
“Kwangu mimi kama mchezaji nimekuja hapa nikiwa mwenye njaa ya kupata mafanikio zaidi na kutumia vizuri muda wangu nikiwa na klabu hii kubwa,” alisema Rice.
Arteta alisema kwamba Rice ataipa nguvu na kutoa mwelekeo wa timu hiyo katika eneo la kati, jambo ambalo limekosekana na hivyo tayari ameanza kuonekana kama ndiye ‘Vieira’ (Patrick) mpya. Vieira alikuwa nahodha na kiungo tishio katika zama za mafanikio ya Arsenal miaka ya 2000.