Na mwandishi wetu
Siku chache baada ya Nelson Okwa kuachwa Simba na kuwashutumu viongozi kwa kuwapangia makocha wachezaji katika mechi, Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu amewaomba mashabiki kutowasikiliza wachezaji wanaoachwa.
Mangungu (pichani) badala yake amewaomba mashabiki hao kubariki maamuzi ya viongozi wao ambao wana lengo la kuwajengea timu ya ushindi.
Juzi, mmoja wa wachezaji aliyeachwa kwenye kikosi chao, Okwa raia wa Nigeria aliwashutumu viongozi wa Simba akidai wamekuwa wakiwapangia makocha wachezaji katika mechi.
Mangungu alieleza kusikitishwa na kauli za Okwa lakini akawataka mashabiki pia kumpuuza sababu mchezaji huyo ni kati ya wachezaji waliopewa nafasi kubwa lakini hakuonesha kile walichokitarajia.
“Hatukatai kukoselewa sababu ndio maana nzuri ya kutambua madhaifu yetu lakini wanachama na mashabiki wetu hawapaswi kuzipa nafasi hizo kelele badala yake watuache viongozi wao tupambane kwa ajili ya kuwajengea kikosi bora kitakachowapa mafanikio msimu ujao,” alisema Mangungu.
Kiongozi huyo alisema tangu kuanza kwa mchakato wa mabadiliko, Simba ndio timu ambayo inaendeshwa kwa uwazi mkubwa nchini ndio maana anapingana na tuhuma za mchezaji huyo sababu aliyeondolewa kwenye timu hayuko peke yake.
Alisema malengo ya Simba ni makubwa na yanahitaji mchezaji ambaye yupo tayari kupigania na kuvuja jasho kwa ajili ya walichokikusudia.
“Sasa ikitokea mtu anapewa nafasi na anashindwa kuonesha msaada wake lazima tutamuondoa ili kuleta mtu sahihi,” alisema Mangungu.
Katika hatua nyingine Mangungu pia amewaomba wanachama na mashabiki wa timu hiyo kuongeza mshikamano ili kujenga umoja utakaowawezesha kutimiza malengo yao msimu ujao.