Munich, Ujerumani
Klabu ya Bayern Munich imetetea uamuzi wa kumfuta kazi aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wake klabu hiyo, Oliver Kahn ingawa Kahn amechukizwa na uamuzi huo akidai kafanyiwa kitu kibaya.
Bayern ilitangaza kumfuta kazi Kahn dakika chache baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya FC Cologne na kutwaa taji la Ligi Kuu Ujerumani au Bundesliga na Kahn akidai kukatazwa kwenda na timu mjini Cologne kufurahia taji hilo na wachezaji.
Mwingine aliyefutwa kazi na Kahn ni mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo, Hasan Salihamidzic na muda huo huo klabu hiyo ikamtangaza Jan-Christian Dreesen kuwa CEO mpya.
Wakati Kahn akilalamikia uamuzi huo, rais wa klabu hiyo, Herbert Hainer amejitetea akidai ulikuwa uamuzi sahihi na kwamba Kahn na Salihamidzic waliarifiwa mapema juu ya uamuzi huo.
Heiner alisema kwamba timu yao haikucheza kwa namna ambayo wangependa iwe na walitilia shaka uwezo wa Kahn na Salihamidzic kubadili mambo katika timu hiyo.
Kwa Kahn namna uamuzi huo ulivyochukuliwa ni kama vile umefunika sherehe za ubingwa ikiwamo ule wa timu ya wanawake ambayo ilikuwa katika kujiandaa na mechi yake ya Jumapili dhidi ya Turbine Potsdam kabla ya kutwaa ubingwa.
Kahn alitumia mtandao wa Twitter kulalamika akidai kwamba ilikuwa siku mbaya katika maisha yake kwa kunyimwa nafasi ya kusherehekea ubingwa na watu wake.
Hainer hata hivyo alisema kwamba Kahn na Salihamidzic wote walipewa taarifa juu ya uamuzi huo siku ya Alhamisi na Salihamidzic aliuchukulia vizuri uamuzi huo na kusafiri na timu hadi Cologne ingawa kwa Kahn mambo hayakuwa hivyo.
“Ni jambo lililotugusa na mwishowe hatukuweza kukubaliana na Oliver lakini yote kwa yote tulimaliza kwa kukubaliana na Ijumaa tulikaa na bodi katika kikao cha dharura na kuamua kumfuta kazi Oliver Kahn, ni kweli Jumamosi hakwenda Cologne kufurahia ubingwa.” alifafanua Hainer.
Kahn alipingana na hoja kwamba alichukia na kujawa hasira baada ya kuarifiwa kwamba klabu hiyo imemfuta kazi.
“Yalikuwa mazungumzo yaliyojaa utulivu, Jumamosi asubuhi nikapata ujumbe kwamba siwezi kwenda kwenye mechi mjini Cologne, niliukubali uamuzi kiungwana, japo ni kweli nilisikitishwa lakini nina furaha hasa baada ya kubeba taji, nina furaha na timu, kocha na mashabiki,” alisema Kahn kipa wa zamani wa Bayern na timu ya Taifa ya Ujerumani.