Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa PSG, Lionel Messi amejikuta katika wakati mgumu baada ya kuzomewa na mashabiki wake jana Jumamosi katika mechi dhidi ya Ajaccio licha ya timu yake kushinda kwa mabao 5-0
PSG ambayo inaelekea kubeba taji la Ligi 1 msimu huu, ushindi huo umeifanya ifikishe pointi 81 zikiwa zimebakia mechi tatu kabla ya msimu wa ligi hiyo kufikia tamati huku Ajaccio ikishuka rasmi daraja.
Katika mechi hiyo, PSG ambao ni vigogo wa jiji la Paris walineemeka kwa mabao ya Fabian Ruiz, Achraf Hakimi, Mohamed Youssouf aliyejifunga na Kylian Mbappe aliyefunga mabao mawili.
Messi ambaye hivi karibuni alisimamishwa wiki mbili na timu yake baada ya kwenda Saudi Arabia kwa shughuli za kibiashara bila ya ruhusa ya klabu na kukosa mazoezi, alianza kuzomewa mara tu baada ya jina lake kutajwa kati ya wachezaji waliopangwa kucheza mechi hiyo.
Mashabiki wa PSG waliojazana kwenye dimba la Parc des Princes, baada ya hapo walimzomea kwa mara nyingine mchezaji huyo baada ya kugusa mpira kwa mara ya kwanza.
Messi ambaye pia ni nahodha wa timu ya Taifa ya Argentina iliyobeba taji la dunia Desemba mwaka jana, alifutiwa adhabu ya kusimamishwa baada ya kuwaomba radhi wachezaji wenzake pamoja na viongozi wake.
Mechi ya jana ilikuwa ya kwanza kwa mchezaji huyo tangu kufutiwa adhabu hiyo baada ya kukosa mechi iliyopita dhidi ya Troyes ambayo PSG ilishinda kwa mabao 3-1.
Msimu huu ndio wa mwisho kwa Messi ambaye bado haijajulikana atajiunga na timu gani ingawa anatajwa kuwaniwa na klabu za Al Hilal ya Saudi Arabia, Inter Miami ya Marekani pamoja klabu yake ya zamani ya Barca ambayo inadaiwa kumtaka arudi kwa mara nyingine.
Kimataifa Mashabiki PSG wamzomea Messi
Mashabiki PSG wamzomea Messi
Read also