Na mwandishi wetu
Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT) limeteua mabondia 22 wanaume na wanawake kujiandaa na mashindano ya kimataifa ya kanda ya tatu Afrika yatakayofanyika nchini kuanzia April 18-22, mwaka huu.
Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga (pichani) alisema kuwa uteuzi huo umefanyika baada ya mchujo wa mashindano na kuwapata hao waliofanya vizuri watakaochuana na mataifa mengine 13.
“Mchujo huu umefanyika katika ukumbi wa mazoezi wa timu ya ngumi ya JKT Mgulani ambapo kati ya idadi hiyo, wanaume ni 16 na wanawake ni sita waliochaguliwa miongoni mwa 56 waliokuwa katika maandalizi,” alisema Mashaga.
Mashaga alisema mabondia walioteuliwa watafanya mazoezi katika kituo cha JKT Mgulani na kwamba Kamati ya BFT ilichagua kituo hicho kutokana na kuwepo kwa miundombinu mizuri ya kufanya mazoezi ya ngumi kwa ufanisi.
Nchi nyingine zitakazoshiriki mashindano hayo ni Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Ethiopia, Somalia, DR Congo, Congo Brazaville, Afrika ya Kati, Gabon, Cameroon na Guinea ya Ikweta.
Mabondia walioteuliwa kwa wanaume ni Karim Juma, Yohana Keneth, Abdallah Salum, Hassan Waziri, Rashid Mrema, Alex Isendi, Mohamed Swalehe, Atanas Ndiganya, Joseph Philip, David Chanzi, Joshua Shadrack, Alphonce Abel, Yusuf Changalawe, Nizza Abdalahamani, Jofrey Peter na Alex Sitta.
Kwa upande wa wanawake ni Rahma Maganga, Mariam Richard, Shakila Abdallah, Aisha Idd, Leyla Yazidu na Beatrice Ambrose.
Timu hiyo itaongozwa na walimu Samwel Batman, Hassan Mzonge, Mussin Mohamed, Rogata Damian, Undule Lang’son na Haji Abdallah huku kamati ya ufundi ikiwa chini ya Michael Changarawe kutoka Mwanza na Robert Suluhu wa Dar es Salaam.