Na mwandishi wetu
Si Yanga si Simba, ndio matokeo ya mechi ya watani wa jadi katika mechi ya Ligi Kuu iliyopigwa jioni ya leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Matokeo hayo ya sare ya bila kufungana yanaifanya kila timu kuambulia pointi moja huku Yanga kwao ikiwa sare ya pili wakati kwa Simba hiyo ni sare ya tatu. Yanga ikiendelea kushika usukani na pointi 20 na Simba ikishika nafasi ya pili na pointi 18.
Nje ya matokeo hayo, mechi hiyo ya watani wa jadi imeendelea kuwa burudani ya aina yake kutokana na ushindani ambao umeonyeshwa na wachezaji wa timu hizo.
Katika mechi ya leo, mbali na matukio kadha wa kadha ya kuvutia, tukio mojawapo ambalo linaendelea kuwa mjadala miongoni mwa mashabiki wa timu hizo ni lile la beki Joash Onyango wa Simba na mshambuliaji Fiston Mayele wa Yanga.
Katika kilichoonekana tangu mwanzo wa mchezo huo ni kama vile Onyango alipania kumuweka katika wakati mgumu Mayele kama ambavyo hali hiyo ilianza kujionyesha katika dakika ya 20 ya mchezo huo pale Mayele alipopenyezewa pasi na kukabiliana ana kwa ana na Onyango kwa kasi huku kila mmoja akiwania mpira uliokuwa mbele yao lakini alikuwa ni Onyango aliyemzidi Mayele na kuondoa hatari langoni mwake.
Tukio jingine la wawili hao lilijitokeza kama dakika nne hivi baadaye ambapo safari hii, Mayele baada ya kuunasa mpira aliupenyeza katikati ya miguu ya Onyango ambaye ilibidi atumie akili ya mpira kwa kumzuia Mayele kwenye njia na mwamuzi kuipa Simba mpira wa adhabu na kumpa Onyango kadi ya njano kwa kosa hilo.
Dakika ya 33 tena, Mayele na Onyango walikutana wakiwania mpira wa juu ambao ulielekezwa kwa Mayele lakini katika kukimbia huko wakiwa pamoja, Onyango alitumia mwili na kumtoa Mayele kwenye mstari kwa bega. Mayele ambaye alikuwa kwenye kasi alijikuta akishindwa kuutumia mpira huo kuleta madhara kwenye lango la Simba.
Dakika ya 43 tena, Mayele aliunganishiwa mpira wa juu ambao kipa wa Simba, Aishi Manula aliouna lakini hesabu zake za kuudaka zilishindikana baada ya kuteleza na hivyo kumpa Mayele nafasi ya kuuwahi na hapo hapo Onyango akawa akimfukuzia lakini akiwa ameshauzuia mpira vizuri Mayele naye akataleza na hivyo ikawa rahisi kwa Onyango kuondoa hali ya hatari langoni mwake.
Hata hivyo mpambano wa wawili hao haukufika dakika zzote 90 za mchezo kwani katika dakika ya 83, Mayele alikwenda benchi.
Nje ya matukio hayo timu zote zilijitahidi kucheza soka la kusomana na mashambulizi ya hapa na pale lakini hadi mwisho wa mchezo hakuna timu iliyotoka uwanjani na bao.
Soka Mayele, Onyango watoana jasho
Mayele, Onyango watoana jasho
Related posts
Read also