Na mwandishi wetu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezitakia heri timu za Simba na Yanga kwenda kuwakilisha vyema katika mashindanoo ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.
Simba itaanza kampeni zake za hatua ya makundi kesho Jumamosi ugenini dhidi ya Horoya AC ya Guinea, mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Jenerali Conte mjini Conakry huku Yanga ikitarajiwa kucheza na US Monastir ya Tunisia siku inayofuata.
Akizungumza wakati akitoa hotuba ya kuahirisha mkutano wa 10 wa Bunge jijini Dodoma leo, Majaliwa alisema hana mashaka na viwango vya timu hizo huku akisema Simba wanatakiwa kuhakikisha wananyunyiza kwa kuwafunga mabao mengi wapinzani wao na Yanga ikatetemesha kwa Watunisia.
“Niwatakie kila heri klabu zetu katika hatua za makundi katika michezo yao ya ugenini, Yanga itakuwa huko Tunisia tunataka mtetemeshe Watunisia na tunawatakia heri Simba wanaocheza klabu bingwa Guinea, nawapa ujumbe wanyunyize hao walale kwa mabao mengi,”alisema.
“Hatuna mashaka na viwango vyenu, Simba nyie ni miongoni mwa klabu 10 bora Afrika,”alisema.
Timu hizo zinazowakilisha Tanzania, baada ya michezo yao ya kwanza hatua ya makundi zitarejea Dar es Salaam kucheza michezo mingine, Simba itakipiga Raja Casablanca ya Morocco na Yanga itacheza na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wiki ijayo kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Soka Majaliwa azitakia heri Yanga, Simba
Majaliwa azitakia heri Yanga, Simba
Related posts
Read also