Na mwandishi wetu
Timu ya Singida Big Stars imeeleza inatambua ubora ilionao sasa timu ya Ihefu ndiyo maana imekwenda Mbeya mapema kujipanga kwa ajili ya mechi hiyo inayotarajiwa kupigwa Februari 12 kwenye Uwanja wa Highlands Estate, Mbarali.
Ofisa Habari wa Singida Big, Hussein Masanza amesema kuwa wapo kwenye maandalizi ya mapema wakitambua ubora wa kikosi cha Ihefu na upinzani wanaokutana nao timu hizo zinapokutana tangu walipokuwa wote Ligi ya Championship.
“Tunaitazama kama mechi ya ushindani mkubwa, unafahamu Ihefu sasa wapo kwenye ubora wametoka nafasi ya 16 mpaka ya saba, wamefanya usajili mzuri dirisha dogo, kwa hiyo hatuitazami hiyo mechi kwa udogo ndio maana tayari timu imetangulia Mbeya mapema.
“Upinzani wetu na Ihefu umekuwepo tangu huko Championship, kila tunapokutana huwa si mechi rahisi hata kidogo, utakuwa mchezo mzuri wa ushindani lakini tuna malengo yetu tunataka kuyafikia ndio maana nguvu kubwa imeelekezwa kwenye mechi hiyo,” alisema Masanza.
Katika mechi ya kwanza baina ya timu hizo, Ihefu ilikubali kipigo cha bao 1-0 ugenini, safari hii timu hizo zinakutana zikiwa kwenye matokeo ya kufanana wote wakiwa wameshinda mechi nne katika michezo yao mitano ya mwisho na kufungwa mmoja kila mmoja.
Singida inashika nafasi ya nne kwa pointi 43 wakati Ihefu ipo nafasi ya saba kwa pointi zake 26 baada ya wote kucheza mechi 22, zikisalia mechi nane kabla ya kumalizika ligi.
Soka Singida Big wakiri, Ihefu wako vizuri
Singida Big wakiri, Ihefu wako vizuri
Related posts
Read also