Paris, Ufaransa
Rais wa Shirikisho la Soka Ufaransa (FFF), Noel le Graet amelazimika kung’atuka katika nafasi hiyo kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili za udhalilishaji kijinsia na ubabe.
Tangu Oktoba mwaka jana Serikali ya Ufaransa imekuwa ikifanya uchunguzi baada ya kupata taarifa za tuhuma hizo ambazo hata hivyo Le Graet amezikana.
Uamuzi wake wa kukubali kujiweka pembeni umekuja baada ya wito kutolewa kila kona kumtaka afanye hivyo kutokana na kauli aliyoitoa kuhusu mwanasoka wa zamani wa Ufaransa, Zinedine Zidane.
Le Graet mwenye umri wa miaka 81, alinukuliwa akisema kwamba asingeweza hata kupokea simu ya Zidane baada ya mwanasoka huyo wa zamani kuhusishwa na mpango wa kuwa kocha wa Ufaransa ingawa baadaye aliomba radhi kwa kauli hiyo aliyosema haikuwa nzuri.
Juzi Jumanne kiongozi wa Kamati ya Maadili ya FFF, Patrick Anton alimtaka Le Graet ajiuzulu wakati mshambuliaji wa Ufaransa Kylian Mbappe na waziri wa michezo, Amelie Oudea-Castera walidai kwamba kiongozi huyo alikosa heshima.
Taarifa ya FFF iliyopatikana jana Jumatano jioni ilieleza kuwa katika kikao cha dharura kilichofanyika jana hiyo hiyo mapema, Le Graet alikubaliana na kamati ya utendaji ya shirikisho hilo kukaa pembeni hadi uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili utakapokamilika.
Uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili Le Graet unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi huu huku Mkurugenzi Mkuu wa FFF, Florence Hardouin naye amesimamishwa katika hatua muhimu za kuendelea na uchunguzi huo na nafasi za wawili hao zitashikwa kwa muda na makamu rais wa FFF, Philippe Diallo.
Kimataifa Bosi wa soka Ufaransa ang’atuka
Bosi wa soka Ufaransa ang’atuka
Related posts
Read also