London, England
Kocha Pep Guardiola amesema muda wake katika klabu ya Man City utakuwa haujakamilika kama atashindwa kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL).
Pep tayari ameongeza mkataba na Man City na sasa atakuwa na klabu hiyo hadi mwaka 2025 akiwa tayari ameiwezesha timu hiyo kutwaa mataji tisa tangu ajiunge nayo mwaka 2016 lakini hajawahi kubeba taji lolote la Ulaya akiwa na timu hiyo.
Mwaka 2021 nusura wabeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini wakafungwa na Chelsea katika mechi ya fainali licha ya matumaini makubwa yaliyokuwapo kwa timu hiyo.
Msimu uliopita, Man City ilipambana hadi hatua ya nusu fainali ikashindwa kutamba mbele ya Real Madrid na misimu mitatu kabla waliishia robo fainali ingawa kabla ya hapo hali ilikuwa mbaya zaidi kwa timu hiyo iliyoishia hatua ya 16 bora kabla ya kushindwa kutamba mbele ya Monaco.
“Si taji hilo tu lakini ni lazima nifikirie kwamba hilo ni taji ambalo tunataka kulishinda na wakati wangu hapa utakuwa haujakamilika kama hatutashinda taji hilo,” alisema Pep.
“Nitafanya kila kitu kwa wakati tutakaokuwa hapa pamoja lakini nilishasema hapo kabla kwamba hilo ni taji ambalo hatuna na tutajaribu kulishinda, nina mtazamo kwamba litapatikana hivi karibuni au hapo baadaye,” alisema.
Katika hatua nyingine, Pep alimpongeza mshambuliaji wake mwenye umri wa miaka 22, Julian Alvarez kwa mchango wake mkubwa kwenye timu ya Argentina iliyotwaa taji la dunia Jumapili iliyopita. Pep pia alimpongeza mchezaji wake wa zamani wa Barcelona Lionel Messi kwa mafanikio hayo pamoja na beki wa zamani wa Man City, Nicolas Otamendi.