Doha, Qatar
Kocha wa Ureno, Fernando Santos amemtupa benchi staa wake, Cristiano Ronaldo katika mechi na Switzeland na kumpa nafasi hiyo, Goncalo Ramos ambaye amemjibu kwa mabao matatu (hat trick) hali inayoacha maswali kuhusu majaliwa ya Ronaldo katika kikosi cha kwanza cha Ureno.
Ureno jana Jumanne iliigubiza Switzerland mabao 6-1 na kufuzu hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia huku kukiwa na utata kuhusu Ronaldo ambaye kocha wake alichukizwa kwa jinsi alivyoonyesha kuchukia na kutoa kauli ya hovyo baada ya kutolewa katika mechi dhidi ya Korea Kusini.
Hii ni mara ya kwanza kwa Ronaldo kukosekana katika kikosi cha kwanza katika mechi 31 za michuano mikubwa akiwa na timu ya Ureno tangu mwaka 2008. Na ingawa jana aliingia dakika ya 74 lakini tayari Ureno ilikuwa imetawala mchezo na kuibugiza Switzerland mabao ya kutosha.
Alichofanya kocha Santos ni kumpa nafasi Ramos, mshambuliaji wa Benfica mwenye umri wa miaka 31 ambaye hakufanya ajizi kuibeba Ureno ambayo sasa inasubiri kuumana na Morocco katika mechi ya robo fainali.
Ramos alifunga mabao yake katika dakika za 17, 51 na 67 wakati mabao mengine yalifungwa na beki mkongwe wa Ureno mwenye miaka 39, Pepe na Guerreiro na Rafael Leao waliohitimisha karamu ya mabao huku bao pekee la Switzerland likifungwa na beki wa Man City, Manuel Akanji.
Mabao ya Ramos hayaishii tu kuwa hat trick ya kwanza kwa mchezaji huyo kwenye fainali za Kombe la Dunia bali pia imempa faraja kubwa kocha wake Santos ambaye bila shaka sasa atakuwa na kila sababu za kumuamini huku maswali yakibaki kuhusu nafasi ya Ronaldo.
Inawezekana hata nafasi aliyopewa Ronaldo katika mechi hiyo ilichangiwa kwa kiasi fulani na kelele za mashabiki wa Ureno waliosafiri hadi Qatar si tu kwa ajili ya kushuhudia fainali za Kombe la Dunia bali pia kuona mastaa wakionyesha ubora wao akiwamo Ronaldo.
Kitendo cha Ronaldo kuonyesha ishara ya kukasirika baada ya kutolewa katika mechi na Korea Kusini na kumtamkia kocha wake maneno ya hovyo kwa kumwambia, ‘ana haraka ya kumtoa’ kilimtia hasira kocha huyo na akamjibu kwa kumuweka benchi na kwa bahati iliyoje, Ramos aliyepewa nafasi hiyo amefanya vizuri.
Swali ni je Ronaldo atakubali kuwa mchezaji wa kuanzia benchi? Na nafasi yake kiujumla ipoje ndani ya kikosi cha Ureno baada ya ushindi dhidi ya Switzerland? Kocha ataamua.
Huu utakuwa mzozo wa pili kwa Ronaldo katika siku za karibuni, tayari ameachana na klabu ya Man United akiwa ametofautiana na kocha wa timu hiyo, Erik ten Hag sababu mojawapo kubwa ikiwa ni kutokubali kuwekwa benchi.
Kimataifa Ronaldo aacha maswali Ureno ikifuzu
Ronaldo aacha maswali Ureno ikifuzu
Related posts
Read also