Na mwandishi wetu
Yanga imetinga hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuifunga Club Africain ya Tunisia bao 1-0, ushindi ambao pia unafuta uvumi na swali la baadhi ya mashabiki kuhusu hatma na uwezo wa kocha Nasreddine Nabi ambaye katika siku za karibuni ajira yake Yanga ilikuwa ikijadiliwa.
Haikuwa rahisi kwa Yanga kupata matokeo hayo kwani ikiwa ugenini Uwanja wa Olympique Rades, Tunis iliingia ikiwa vichwa chini baada ya suluhu waliyoipata kwenye mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Kumbukumbu mbaya
Mbali ya kuwa na kibarua kigumu ugenini, bado timu hiyo ilikuwa na kumbukumbu mbaya ya mechi yao ya mwisho ya kimataifa dhidi ya Al Hilal ya Sudan ambapo Wanajangwani hao waliondolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuangukia Shirikisho.
Katika mechi ya kwanza na Hilal iliyopigwa kwa Mkapa iliisha kwa sare ya bao 1-1 na ilipokwenda Sudan kwa mechi ya marudiano, Yanga ilifungwa bao 1-0 hivyo kung’oka kwa kufungwa mabao 2-1.
Yanga hata hivyo ilionesha ukomavu wake na kuamua kuustaajabisha umma, kupindua meza ugenini na kujifariji kwa matokeo ya huzuni waliyoyapata mara ya mwisho kwa kuiadhibu Africain nyumbani kwao.
Baada ya miaka sita yarejea kwa kishindo
Yanga ilikuwa ikitumaini mno msimu huu kuvunja rekodi yake ya miaka 24 ya kutoingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwani ilifanya hivyo mara ya mwisho mwaka 1998 lakini haikuwa hivyo baada ya Hilal kuwapokonya tonge mdomoni dakika za mwisho.
Lakini sasa kwa kuingia makundi Kombe la Shirikisho imeifanya irejee kwa kishindo katika hatua hiyo tofauti na ilivyofanya mara ya mwisho miaka sita iliyopita ilipotinga makundi baada ya kuifurumusha Sagrada Esperanca ya Angola.
Dhidi ya Esperanca, Yanga ilifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-0 ikiwa nyumbani. Mabao yaliyowekwa kimiani na Simon Msuva na Matheo Anthony.
Ilipoenda ugenini ilifungwa bao 1-0 na hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 2-1 lakini safari hii imetinga kwa ushindi wa ugenini tena nyumbani kwa Waarabu, ni kishindo cha aina yake!
Yaweka heshima kwa taifa
Ushindi wa Yanga umeifanya Tanzania kuwa nchi pekee Afrika Mashariki kuwa na timu mbili kwenye michuano ya ngazi ya klabu Afrika.
Simba ilishatangulia mapema kwenye makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikisubiri kupangwa kwa droo hiyo baada ya kuifunga Nyassa Big Bullets ya Malawi kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-0 kisha kuichapa Primeiro de Agosto ya Angola kwa mabao 4-1.
Kiujumla Yanga imekuwa timu ya tatu kufika hapo baada ya awali timu ya wanawake ya Simba Queens kuwakilisha vyema kama timu pekee kutoka Ukanda wa Cecafa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake kabla ya kufungwa na mabingwa watetezi Mamelodi Sundowns bao 1-0 kwenye nusu fainali iliyopigwa jana nchini Morocco.
Thamani ya Aziz Ki
Ukiachana na kujitoa kwa wachezaji wa Yanga katika mechi hiyo, ikionekana kila mmoja akifanya jukumu lake kwa uwezo wa juu kama ilivyokuwa kwa kipa Djigui Diarra, kiungo Aboubakary Salum ‘Babu Kaju’, Bernard Morrison na wengine lakini ilikuwa ni Stephanie Aziz Ki aliyewatoa Yanga machozi ya furaha.
Awali katika mechi ya iliyopigwa kwa Mkapa, Aziz Ki hakuonesha kiwango kilichotarajiwa na wengi ambapo baada ya mechi alilaumiwa na baadhi ya mashabiki kwa madai kwamba hakuwa na msaada uliotarajiwa.
Jana, Aziz alianzia benchi kabla ya kuingia dakika ya 68 kuchukua nafasi ya Khalid Aucho na dakika ya 78 alifunga bao zuri akiunganisha mpira uliotengwa kwa kichwa na Fiston Mayele.
Baada ya bao hilo, Aziz Ki alionekana shujaa, mkombozi, mbabe wa vita, fundi na majina mengi ambayo alitukuzwa usiku huo lakini mwisho aliwakumbusha watu kuweka akiba ya maneno na kuifanya kazi aliyotumwa wakati anatua Jangwani akitokea Asec Mimosas ya Ivory Coast.
Bado mna swali kwa Nabi?
Kabla ya mechi vuguvugu kubwa lilikuwa ni mashabiki wa Yanga kutoridhishwa na mwenendo wa timu hiyo kwenye michuano ya Afrika. Zigo kubwa la lawama alibebeshwa kocha wa timu hiyo, Nasreddine Nabi huku tetesi za kufungashiwa virago zikiibuka mpya kila kukicha. Presha ilikuwa kubwa mno.
Kila mmoja aliamini mwisho wa Nabi pale Yanga umefika na mechi hiyo dhidi ya Africain pengine ndiyo ilikuwa tiketi yake lakini mwisho Nabi raia wa Tunisia hakupindua meza tu dhidi ya nduguze hiyo jana bali pia alipindua mawazo ya mashabiki wengi wanaofahamu kukosoa tu!
Na sasa baada ya yote, nafikiri mashabiki na wadau waliokuwa wakihoji uwezo na falsafa za Nabi wakikutana na uso wa kocha huyo hapana shaka utakuwa wenye tabasamu lenye maswali juu yao kwamba, bado wana swali juu ya ‘uprofesa’ wake?
Soka Bado mna swali kwa Nabi?
Bado mna swali kwa Nabi?
Related posts
Read also