London, England
Beki wa kushoto wa Chelsea na timu ya Taifa ya England, Ben Chilwell huenda akazikosa fainali za Kombe la Dunia baada ya kuumia jana Jumatano usiku wakati akiiwakilisha Chelsea kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Dinamo Zagreb.
Chilwell mwenye umri wa miaka 25 aliumia misuli ya mguu katika dakika za nyongeza na kushindwa kuendelea na mechi hiyo ambapo baadaye alipigwa picha akitoka katika dimba la Stamford Bridge huku akichechemea akiwa ameshikwa ingawa timu yake ilitoka na ushindi wa mabao 2-1 katika mechi hiyo.
Kwenye fainali za Euro 2020, Chilwell alikuwa katika kikosi cha England ingawa hakupata nafasi ya kucheza na sasa anajikuta akipata pigo la pili katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja, Novemba mwaka jana aliumia na kulazimika kuwa nje ya uwanja hadi Mei mwaka huu.
Alipoulizwa iwapo mchezaji huyo anaweza kuzikosa fainali za Kombe la Dunia, Potter alisema, “Nafikiri tunaweza kusema hivyo, japo sitaki kusema zaidi ya hilo lakini inapotokea kwa mchezaji kutoka kwa kujikokota kama alivyofanya, hilo haliwezi kuwa jambo lenye ishara nzuri.”
“Ni pigo kwetu na pigo kwake, inasikitisha hatokuwa yeye tu aliyeathiriwa na hilo katika kipindi hiki kwa sababu Oktoba imekuwa na changamoto zake kwa mechi ambazo tunatakiwa kucheza lakini hivyo ndivyo inavyotakiwa kuwa,” alisema Potter.
Kocha wa zamani wa England, Glenn Hoddle akimzungumzia mchezaji huyo alisema, “Namsikitikia Ben, inaumiza, kuna wakati unapokuwa na matatizo ya misuli kunakuwa na dalili za kutahadharisha, hapo ndipo unapolazimika kuinua mikono, ndivyo ilivyokuwa kwake, sura ilijionyesha, alipogusa mpira alianza kulalamika na kuonekana mwenye maumivu makali, sijui ni kwa nini hawakumbeba.”
Fainali za Kombe la Dunia zitaanza kutimua vumbi Qatar Novemba 20 ambapo England itatupa kete yake ya kwanza siku inayofuata kwa mechi dhidi ya Iran. Chilwell hadi sasa ameichezea England mara 17.
Kimataifa Beki Chelsea hatihati Kombe la Dunia
Beki Chelsea hatihati Kombe la Dunia
Related posts
Read also