London, England
Kocha mpya wa Brighton, Roberto de Zerbi amesema alizungumza na kocha wa Manchester City, Pep Guardiola kabla ya kukabidhiwa kibarua cha kuinoa timu hiyo na kocha huyo ameahidi kumpa msaada.
De Zerbi mwenye umri wa miaka 43 amesaini mkataba wa miaka minne kuinoa timu hiyo akichukua nafasi ya Graham Potter ambaye kwa sasa anainoa Chelsea akichukua nafasi iliyoachwa na Thomas Tuchel aliyetimuliwa kutokana na matokeo mabaya ya timu hiyo.
“Nilizungumza na Pep Jumapili jioni, amefurahi kusikia ninaanza kazi hapa, aliniambia mambo mazuri kuhusu klabu hii na kama nitahitaji msaada atakuwa mwenye furaha kunisaidia, lakini si wakati tunapocheza dhidi yao,” alisema kocha huyo Mtaliano.
De Zerbi pia alisema kwamba aliamua kuichagua timu hiyo kwa sababu alikuwa akiitaka Ligi Kuu England licha ya kuwa na fursa nyingine nyingi.
“Brighton walinihitaji hasa niwe kocha na aina ya uchezaji wao ipo sawa na mtazamo wa soka langu, tulikutana mara moja mara baada ya mazungumzo, ni kweli kwamba kuna timu nyingine zilinitaka lakini nina furaha kuwa hapa,” alisema De Zerbi.
De Zerbi alikuwa hana kazi baada ya kuachana na klabu aliyokuwa akiinoa ya Shakhtar Donetsk ya Ukraine, na alichukua uamuzi wa kuondoka baada ya Urusi kuivamia Ukraine kijeshi.
“Ni kweli kwamba sikutarajia kumalizana nao kwa kila kitu mwezi Februari na ni kweli kwamba haikuwa vizuri, si kwa sababu tu ya vita bali haikuwa vizuri kuliacha jambo ambalo linakwenda vizuri,” alisema De Zerbi.
“Ninachoweza kufanya ni kuendelea kufanya kazi kwa hamasa ile ile, ni kweli kwamba nina uzoefu lakini nawafikiria watu wa Ukraine na wachezaji niliokuwa nawafanyisha mazoezi,” alisema De Zerbi.
Kocha huyo ambaye wakati wote alikuwa akizungumza kwa kumtumia mkalimani katika mkutano wake na waandishi wa habari na ingawa taarifa yake ya awali alizungumza Kiingereza, amesisitiza kwamba lugha haiwezi kuwa kikwazo katika kazi yake.
“Samahani kwa Kiingereza changu, lengo langu ni kuanza kuzungumza Kiingereza itakapofika Januari, nina furaha kuwa hapa, kuwa kocha mkuu mpya na nataka kumshukuru mwenyekiti na klabu kwa ujumla, nimemsoma kila mchezaji na nitafanya kazi nzuri,” aliongeza.
Brighton kwa sasa inashika nafasi ya sita kwenye Ligi Kuu England na haijacheza mechi yoyote tangu kuondoka kwa Potter baada ya mechi zake dhidi ya Bournemouth na Crystal Palace kuahirishwa na sasa huenda ikacheza mechi nyingine mapema mwezi ujao dhidi ya Liverpool.
Kimataifa Pep kumsaidia kocha mpya Brighton
Pep kumsaidia kocha mpya Brighton
Related posts
Read also