London, England
Wazungumzie washambuliaji unaodhani wanaweza kutwaa kiatu cha dhahabu katika Ligi Kuu England, msimu huu, Erling Haaland huwezi kumuweka kando, tayari amelianzisha balaa, ana mabao tisa katika mechi tano.
Kati ya mabao hayo tisa ana hat trick mbili wakati ligi bado mbichi na hivyo anakuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao tisa katika Ligi Kuu England kwenye mechi tano tu za mwanzo.
Japo ni mapema mno kumpamba na kujipa matumaini, lakini kwa rekodi yake hadi sasa Manchester City wana kila sababu ya kujifariji na kutamba kwamba hawajafanya kosa kuipigania saini ya Haaland na ni sahihi kabisa kusema kwamba Man City si tu wamelamba dume bali wamelamba dume la mbegu.
Kocha wa Nottingham Forest, Steve Cooper ambaye timu yake Haaland aliipiga hat trick katika ushindi wa mabao sita ambao City waliupata, akimzungumzia mchezaji hyo anasema, “Yuko vizuri, ana sifa nyingi.”
Ukiweka kando mbio za kuwania kiatu cha dhahabu kwa kasi ya upachikaji mabao aliyoanza nayo Haaland huenda akavunja kila rekodi iliyopo sasa kwani ndio kwanza ana miaka 22 na hivyo bado ana miaka mingi ya kucheza soka la ushindani katika Ligi Kuu England.
Ukiachana na uwezekano wa hilo kwa kasi hii, miaka michache ijayo Haaland anaweza kuwa gumzo duniani kwa kusajiliwa kwa bei mbaya, na hapa tunaiangalia klabu ya Real Madrid ambayo haitopenda kukaa kimya na kumuacha Haaland azeekee Man City wakati klabu hiyo inaamini ana vigezo vyote vinavyohitajika Real Madrid.
Kilichowahi kutokea kwa mastaa wengi waliotamba katika Ligi Kuu England na hatimaye kutimkia Real Madrid kuanzia Steve, Mcmanan, David Beckham, Cristiano Ronaldo, Gareth Bale na wengineo, pengine ndicho ambacho kinasubiriwa kutokea kwa Haaland miaka michache ijayo.
Kuna mambo mawili yanayoweza kuchangia jambo hilo kutokea, moja ni shauku ambayo anaweza kuwa nayo mchezaji huyo kama ilivyo kwa mchezaji mwingine yeyote kutaka changamoto mpya na hivyo haitokuwa ajabu kwa Haaland kutaka changamoto mpya.
Jambo la pili ni nguvu ya pesa ya klabu ya Real Madrid ambayo haitoona tabu kuvunja benki ili tu impate mchezaji wa hadhi inayemtaka, ilipomtaka Bale, kigogo mmoja wa klabu hiyo alinukuliwa akisema kwamba mchezaji huyo (Bale) alizaliwa ili aichezee Real Madrid, bila shaka itakuwa hivyo hivyo kwa Haaland, naye tutaambiwa alizaliwa ili aichezee Real Madrid..
Hata hivyo wakati Haaland akipambwa na kupewa matumaini makubwa, kocha wa Man City, Pep Guardiola ana mawazo tofauti, analifikiria taji la Ligi Kuu England na mengineyo, hasumbuliwi na rekodi za mafanikio anazohusishwa nazo mchezaji huyo mmoja.
“Erling an sifa za kuwa hapo alipo, alichokifanya Norway, Austria na Ujerumani kwa sasa anajaribu kukifanya hapa, namjua kidogo na sijui kama atakuwa mwenye furaha ya kuvunja rekodi kama hatutabeba mataji,” alisema Pep.
Kimataifa Huyu Haaland balaa, mechi 5 mabao 9
Huyu Haaland balaa, mechi 5 mabao 9
Related posts
Read also