Na mwandishi wetu
Klabu ya soka ya Yanga rasmi leo imetangaza kuachana na aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Hassan Bumbuli wakieleza kuwa amemaliza makataba wa kuitumikia klabu hiyo huku kukiwa na habari kwamba majukumu yake sasa yatahamia kwa Taji Liundi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyowekwa kwenye kurasa za mitandao ya kijamii ya Yanga, imemshukuru kwa utumishi wake mzuri kwa kipindi cha miaka alichokuwa na timu hiyo huku ikimtakia kila la heri.
“Ndugu Bumbuli amemaliza mkataba wake wa kuitumikia klabu ya Yanga, hivyo uongozi unamshukuru sana kwa kazi yake nzuri na kumtakia kila la heri na mafanikio katika maisha na kazi zake nje ya klabu ya Yanga,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Hata hivyo, taarifa za kuondoka kwa Bumbuli zilianza kushika kasi tangu alipotambulishwa Haji Manara kuwa Ofisa Habari wa Yanga pia ndani ya kitengo hicho lakini zikarejea tena kwa nguvu hivi karibuni baada ya kuondoka kwa aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mazingiza ikielezwa kuwa uongozi mpya wa timu hiyo unarekebisha baadhi ya vitengo ndani ya klabu hiyo.
Siku moja kabla ya kutoka kwa taarifa hiyo, Bumbuli aliyerithi nafasi hiyo kutoka kwa Dismas Ten mwaka 2019, aliweka andiko la kuwaaga mashabiki na wapenzi wa timu hiyo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.
“Inaelezwa kuwa watu wanaweza kutengeneza nafasi, na niseme kwa dhati kwamba ninyi nyote mmeifanya hii Yanga bora. Inaweza kuwa huzuni kusema kwaheri lakini nina shauku kwa yatakayokuja mbele yangu, kwenu na kwa klabu yangu pendwa.
“Zawadi nzuri mno niliyoipata kufanya kazi na Yanga, kuwatumikia Wananchi. Asanteni kwa ukarimu, hekima na kunitengenezea sehemu niliyokuwa na furaha kutumia saa zangu za kazi na zaidi.
“Kwenu Wananchi sipati maneno ya kueleza jinsi gani gani mlivyo na shukrani! Ninyi ni wa kipekee mno. Nilikuja tukiwa watupu kwenye pesa na makombe, naondoka kukiwa na makombe pamoja na rekodi zilizowekwa. Asanteni kwa kunipa nafasi ya kuwatumikia,” aliandika Bumbuli.
Baada ya kuondoka kwa Bumbuli, Liundi ambaye amewahi kufanya kazi kwenye vyombo mbalimbali vya habari nchini anatajwa kukabidhiwa jukumu hilo ikiwa ni miongoni mwa mabadiliko yaliyofanywa na ambayo huenda yakaendelea kufanywa ndani ya Yanga chini ya rais mpya wa klabu hiyo, Hersi Said.
Soka Bumbuli ampisha Taji Liundi Yanga
Bumbuli ampisha Taji Liundi Yanga
Related posts
Read also