Bellinzona, Uswisi
Rais wa zamani wa Fifa Sepp Blatter na rais wa zamani wa Uefa, Michel Platini wamefutiwa mashitaka ya ufisadi na matumizi mabaya ya ofisi yaliyokuwa yakiwakabili katika mahakama moja ya nchini Uswisi.
Mabosi hao maarufu wa zamani wa soka, walidaiwa kuhusika katika malipo yaliyodaiwa kuwa haramu ya Pauni 1.7 milioni, fedha ambazo Blatter alidaiwa kumlipa Platini wakati Blatter akiwa rais wa Fifa na Platini akiwa rais wa Uefa.
Platini ambaye alikuwa akitarajiwa kuchukua mikoba ya Blatter kwenye kiti cha urais wa Fifa, ilielezwa kwamba alilipwa fedha hizo na Blatter kwa kazi ya kutoa ushauri kwa bosi huyo wa Fifa na ndipo waendesha mashitaka wa Uswisi walipowafikisha mahakamani wawili hao kwa tuhuma za kuwapo mchezo mchafu katika malipo hayo.
Mahakama hiyo ilielezwa kwamba Platini alipewa kazi hiyo na Blatter kuanzia mwaka 1998 hadi 2002 wakati Blatter aliposhika madaraka ya Fifa kwa mara ya kwanza lakini malipo hayo yalifanyika mwaka 2011 na kuibua madai kwamba yalikuwa ni malipo ya kifisadi.
Katika maelezo yao waendesha mashitaka hao wa Uswisi walidai kuwa malipo hayo kwenda kwa Platini hayakuwa halali lakini majaji katika hukumu yao walisema kwamba Blatter na Platini hawakukutwa na hatia yoyote ya kufanya ufisadi kupitia malipo hayo.
Sakata hilo liliwaweka mahala pabaya Blatter na Platini ambao walijikuta wakifungiwa kujihusisha na soka na kuondolewa katika nyadhifa zao na kamati ya maadili ya Fifa na licha ya kukata rufaa lakini kamati ya rufaa ya Fifa ilitupilia mbali rufaa yao, baadaye walikata rufaa katika mahakama ya michezo ambako pia waligonga mwamba.
Awali kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani mwezi uliopita, Blatter mwenye umri wa miaka 85 aliugua ghafla na mahakama ikalazimika kuahirisha kesi lakini baadaye alinukuliwa akisema kwamba malipo aliyoidhinisha kwa Platini yalikuwa halali na yalitokana na maelewano mazuri baina ya marafiki wawili.
Kimataifa Blatter, Platini wafutiwa kesi ya ufisadi
Blatter, Platini wafutiwa kesi ya ufisadi
Related posts
Read also