New York, Marekani
Rapa maarufu duniani, R. Kelly amehukumiwa kwenda jela miaka 30 kwa kosa la kutumia umaarufu na ustaa wake kudhalilisha kijinsia watoto na wanawake.
Hukumu hiyo iliyotolewa jana na mahakama moja jijini New York inakuwa pigo kubwa kwa rapa huyo aliyetamba zaidi miaka ya 1990 na 2000 kwani kwa sasa ana miaka 55 na ambaye pia aliwahi kukutwa na hatia kwa uhalifu wa kujipatia fedha kwa njia zisizo halali na uhalifu wa kingono mashitaka yaliyomuandama kwa muda mrefu.
Akiwa mahakamani kabla ya hukumu kutolewa, kundi la wanawake lilimzunguka kama vile kutaka kumvamia ambapo mmoja wao alinukuliwa akisema, “Nilitamani hata ningekufa kwa hali ambayo ulinifanya niwe nayo.”
Akiwa amevaa mavazi ya wafungwa na miwani ya rangi nyeusi, Kelly alikataa kusema lolote ingawa wakili wake alinukuliwa akisema kwamba wanakusudia kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.
Jaji mmoja katika mahakama hiyo, Ann Donnelly alisema kwamba rapa huyo maarufu alikuwa akitumia ngono kama silaha ya kuwafanya wanawake na watoto kufanya mambo ambayo hayazungumziki na kwa wengine aliwasababishia magonjwa ya zinaa. “Uliwafundisha kuwa mapenzi ni utumwa na vita,” alisema jaji huyo mahakamani hapo.
Mahakama hiyo ilielezwa namna ambavyo Kelly alikuwa maarufu na vibao kama Ignition na I Believe I Can Fly na kuutumia umaarufu alioupata kuwarubuni wanawake na watoto katika mambo ya ngono kwa takriban miaka 20.
Katika maelezo hayo mahakama pia ilielezwa namna ambavyo mwanamuziki huyo alikuwa akiwarubuni na kuwasafirisha wanawake katika majimbo tofauti tofauti ya nchini Marekani akisaidiwa na mameneja wake, walinzi na wasaidizi wengine aliokuwa akiandamana nao kwenye msafara wake.
Mahakama pia ilielezwa namna ambavyo, Kelly alipata kihalali ruhusa ya kimaandishi na kumuona mwanamuziki Aaliyah mwaka 1994 wakati huo Aaliyah akiwa na miaka 15. Aaliyah ambaye pia alikuwa mwanamuziki alifariki kwa ajali ya ndege miaka saba baaadaye.
Ndoa hiyo hata hivyo baadaye ilifutwa baada ya kubainika kwamba kulikuwa na udanganyifu kwa umri wa Aaliyah ambaye taarifa hizo za kimaandishi zilionyesha alikuwa na miaka 18 wakati haikuwa kweli.
Mmoja wa wanamuziki aliyefanya kazi na Kelly, Jovante Cunningham, alisema kwamba hakuwahi kuamini kama ingeweza kufika siku ya leo na hatima ya kesi kufikia hatua hiyo.
“Sikuwahi hata mara moja kuamini kama kuna siku mifumo ya kimahakama italimaliza hili jambo kwa wasichana weusi na weupe, niko hapa najivunia mfumo wangu wa kimahakama, najivunia wahanga wenzangu na nimeridhishwa na uamuzi uliofikiwa.” alisema mdada huyo.
Awali waendesha mashitaka walishauri, Kelly afungwe kifungo kisichopungua miaka 25 jela kutokana na ukubwa wa jinai aliyohusika nayo ili iwe fundisho kwa watu wengine kujihusisha na makosa hayo.
Burudani R Kelly jela miaka 30
R Kelly jela miaka 30
Related posts
Read also