Na mwandishi wetu
Yanga imetoka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Namungo FC katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyopigwa leo Jumanne Mei 13, 2025 kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo Yanga sasa imefikisha pointi 73 katika mechi 27 na kuiacha Simba inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi nne ingawa Simba imecheza mechi 26.
Stephane Aziz Ki ndiye aliyekuwa wa kwanza kuzitikisa nyavu za Namungo katika dakika ya 26 akiitumia pasi ya winga Maxi Nzengeli.
Namungo kabla hawajatulia walipachika bao la pili dakika ya 30 mfungaji akiwa ni Prince Dube ambaye aliitumia vizuri krosi murua ya Kibwana Shomari na kuzifanya timu ziende mapumziko Yanga ikiwa na mabao mawili.
Bao la tatu na la mwisho kwa Yanga lilipatikana kipindi cha pili mfungaji akiwa ni Nzengeli akiitumia pasi ya Israel Mwenda ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Kibwana Shomari.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo zilizochezwa leo, JKT Tanzania iliibugiza Fountain Gate mabao 3-1, mabao ya washindi yakifungwa na Mohamed Bakar, Shiza Kichuya na Edward Songo wakati bao pekee la Fountain likifungwa na William Edgar.
Nayo Pamba Jiji FC iliilaza Ken Gold mabao 2-0 huku mabao ya washindi yote yakipachikwa wavuni na Abdulaye Camara.
Azam FC iliipa kichapo cha nguvu Dodoma Jiji FC kwa kuinyuka mabao 5-0, mabao ya washindi yakifungwa na Lusajo Mwaikenda, Abdul Sopu, Gibril Sillah, Nassor Saadun na Frank Tiese.
Kimataifa Yanga yaicharaza Namungo 3-0
Yanga yaicharaza Namungo 3-0
Read also