Madrid, Hispania
Baada ya Shirikisho la Soka Brazil (CBF) kumtangaza rasmi, Carlo Ancelotti kuwa kocha mkuu mpya wa timu ya nchi hiyo, Ancelotti mwenyewe amesema hajawahi kuwa na tatizo na timu anayoachana nayo ya Real Madrid.
Ancelotti, 65, pia amesema kwamba wakati huu akijiandaa kujiunga na timu ya taifa ya Brazil hataki mpango huo ufanywe kuwa jambo kubwa.
Katika siku za karibuni mambo ya baadaye ya kocha huyo mwenye mkataba na Real Madrid hadi mwaka 2026, yamekuwa yakijadiliwa huku mpango wa kujiunga na Brazil ukitawala mjadala huo.
Wakati CBF wakimtangaza Ancelotti, klabu ya Real Madrid bado haijaweka wazi kuondoka kwa kocha huyo ingawa habari zinadai kwamba klabu hiyo tayari imeshaweka mambo sawa na kocha wa Bayer Leverkusen, Xabi Alonso ili amrithi Ancelotti.
Taarifa ya CBF imeweka wazi kuwa Ancelotti ataachana na Real Madrid mara tu baada ya timu hiyo kucheza mechi yake ya mwisho ya La Liga dhidi ya Real Sociedad na siku yake ya kuanza rasmi kibarua kipya ni Mei 26.
Habari za ndani zinadai kuwa Ancelotti akiwa na timu ya Brazil atakuwa akilipwa Dola 197,000 kwa wiki, kiwango ambacho ni karibu mara mbili ya watangulizi wake, Tite na Dorival Junior.
Inadaiwa kwamba kama kocha huyo ataiwezesha Brazil kubeba Kombe la Dunia mwaka 2026 atapata marupurupu yanayofikia Euro milioni 5.
“Kama nisingekuwa na mkutano na waandishi leo (Jumanne) lingekuwa jambo zuri sana, kuna mambo ambayo siwezi kuyaelezea kwa sasa kwa sababu bado nipo Madrid na nataka kuheshimu jezi hii,” alisema Ancelotti.
Ancelotti alisema kwamba kuanzia Mei 26 na kuendelea atakuwa kocha wa Brazil na kudai kwamba hiyo ni changamoto muhimu kwake lakini angependa amalize hatua ya mwisho ya safari yake ya kipekee na Madrid.
Kocha huyo alisisitiza kwamba hajawahi kuwa na tatizo na Real na hatokuwa na tatizo na Real kwani ni klabu anayoipenda hasa moyoni mwake lakini kila kitu katika maisha kina tarehe ya mwisho.