Na mwandishi wetu
Simba imeendeleza kasi yake ya kulisaka taji la Ligi Kuu NBC ikiilaza Pamba Jiji mabao 5-1 huku Jean Ahoua akipachika mabao matatu (hat trick) na mengine yakifungwa na Leonel Ateba.
Kwa ushindi Simba imezidi kujiimarisha katika nafasi ya pili na pointi 66 ikizidiwa pointi nne na mahasimu wao Yanga wanaoshika usukani, ingawa Yanga imecheza michezo 26 na Simba 25.
Ushindi huo wa leo Alhamisi, Mei 8, 2025, ulianza kupatikana dakika ya 15 kwa bao la Ahoua kwa mkwaju wa penalti baada ya Joshua Mutale kchezewa ndivyo sivyo katika eneo la penalti.
Dakika 20 baada ya bao hilo, Ahoua kwa mara nyingine alizitikisa nyavu za Pamba kwa bao la mpira wa adhabu na kuzifanya timu hizo ziende mapumziko Simba wakiwa mbele kwa mabao 2-0.
Ahoua alifanya yake tena akiandika bao la tatu dakika ya tatu tangu kuanza kipindi cha pili safari hii akiujaza wavuni mpira kwa kichwa kufuatia krosi iliyochongwa ya Elly Mpanzu.
Mambo yalizidi kuwaharibikia Pamba baada ya kufungwa bao la nne na la tano yote yakifungwa na Ateba dakika za 80 na 84 wakati bao pekee la kufutia machozi la Pamba lilifungwa na Mathew Momanyi katika dakika ya 85.
Kwa mabao hayo matatu au hat trick Ahoua pia ameondoka na mpira lakini sambamba na hilo mchezaji huyo pia amefanikiwa kuibuka na tuzo ya mchezaji bora wa mechi hiyo.

Ahoua pia mabao hayo matatu yamembeba na kuwa mchezaji mwenye mabao mengi katika Ligi Kuu NBC akifikisha 15 akifuatiwa na wachezaji wawili wa Yanga, Clement Mzize mwenye mabao 13 na Prince Dube mabao 12.
Ushindi wa leo pia umezidi kuiongezea nguvu Simba katika kulisaka taji la ligi hiyo na mahasimu wao Yanga wanaoshika usukani ambao pia ni mabingwa watetezi.
Simba ambayo katika mechi yake ya mwisho na JKT Tanzania ilishinda kwa bao 1-0, itakuwa na mechi nyingine Jumapili ijayo kwenye uwanja huo huo dhidi ya KMC na kama itaendeleza wimbi la ushindi itakuwa imejitofautisha na Yanga kwa pointi moja.