London, England
Arsenal imechapwa mabao 2-1 na Bournemouth jana Jumamosi katika Ligi Kuu England (EPL) lakini kocha Mikel Arteta hajababaika badala yake ametaka hasira za kipigo hicho zielekezwe Jumatano mjini Paris katika mechi na PSG.
Jumatano Arsenal itakuwa ugenini jijini Paris kuumana na PSG katika mechi ya pili ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo Arteta na wachezji wake watakuwa na kazi ya kipindua meza baada ya kulala kwa bao 1-0 katika mechi ya kwanza.
Katika mechi na Bournemouth, Arsenal ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Declan Rice ambaye hiyo ilikuwa mechi yake ya 100 na timu hiyo lakini baadaye mabao ya Dean Huijsen na Evanilson yalitosha kuipa Bournemouth ushindi.
Akizungumzia matokeo hayo, Arteta aliwaambia waandishi wa habari kwamba timu yake ilichotengeneza ni hali ya hasira, kuvurugwa na kujijengea hisia mbaya.
“Kwa hiyo ni lazima tuhakikishe tunaitumia hali hiyo siku ya Jumatano ili tuwe kwenye kiwango bora mjini Paris, tushinde mechi na kufuzu hatua ya fainali (Ligi ya Mabingwa Ulaya),” alisema Arteta.
Wakati nafasi yao kwenye mbio za taji la EPL zikifutika baada ya Liverpool kulibeba taji hilo, taji jingine wanalolifukuzia sasa ni la Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini kwanza lazima wauvuke mtihani wa PSG hapo Jumatano.
Sambamba na hilo, Arsenal pia ina kazi ya kuhakikisha inazipata pointi sita katika mechi tatu zilizobaki za EPL ili kujihakikishia nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao wa 2025-26.
Arteta amekiri kwamba kwa hali waliyonayo hawafikirii michuano ya Ulaya pekee na katika kuzisaka pointi hizo sita watakuwa na mechi mbili ngumu kuanzia Jumapili ijayo ugenini dhidi ya Liverpool ikifuatiwa na mechi nyingine dhidi ya Newcastle.
“Kimahesabu bado hatujafuzu (kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao), bado hutujaweza kujihakikishia nafasi ya pili, bado tuna kazi kubwa ya kufanya,” alisema Arteta.