Manchester, England
Beki wa Man United, Harry Maguire amesema wachezaji wa timu hiyo wanajiona wenye deni la kombe kwa mashabiki wao kutokana na imani waliyonayo baada ya kupitia katika msimu usio na mafanikio kwenye Ligi Kuu England (EPL).
Kwa mwenendo wa ligi hiyo ulivyo kwa sasa ni wazi Man United itamaliza msimu huu ikiwa katika nafasi za katikati na hii ni mara ya kwanza tangu miaka ya 1990 ingawa kwa upande mwingine timu hiyo inaonekana kurudi katika ubora wao kwenye Europa Ligi.
Baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Athletic Bilbao ugenini Hispania jana Alhamisi, katika mechi ya kwanza ya nusu fainali ya Europa Ligi, Maguire na wachezaji wenzake wapo katika mwelekeo mzuri wa kucheza mechi ya fainali ya ligi hiyo.
Mauire alisema hawana cha kuwaokoa katika msimu huu kwa sababu anafikiri umekuwa msimu wa kukatisha tamaa kwa kuwa wamekuwa na mechi nyingi walizopoteza na wameyumba kwa sana.
“Umekuwa msimu mgumu, wa kukatisha tamaa lakini ndio soka lilivyo, kunakuwa na mambo ya kukumbuka, ni mambo ya kutengeneza vitu vya kukumbukwa, ni suala la kushinda mataji na tuna nafasi kubwa ya kushinda taji,” alisema Maguire.
Maguire alisema kwamba hilo (taji) ni haki ambayo wanatakiwa kupewa mashabiki wa timu hiyo kwani ndicho kitu muhimu kwao.
Kocha wa Man United,r Ruben Amorim tangu aanze kuinoa timu hiyo ameshinda mechi saba kati ya tisa za Europa Ligi lakini katika EPL ameshinda mechi sita tu kati ya 23.
Wakati kocha huyo akijibebesha lawama kwa mwenendo mbaya kwenye ligi tangu ajiunge na timu hiyo Novemba mwaka jana, Maguire amewanyooshea kidole wachezaji wenzake kwa alichosema wana wajibu wa kuendana na mabadiliko ya makocha kutoka Erik ten Hag aliyetimuliwa na Amorim wa sasa.