Na mwandishi wetu
Bao pekee la Maxi Nzengeli limetosha kuibwaga JKU na kuifanya Yanga ibebe Kombe la Mapinduzi leo Alhamisi Mei Mosi, 2025 kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba.
Nzengeli alifunga bao hilo pekee dakika ya 45 baada ya kutengenezewa pasi na Farid Mussa ambapo mfungaji aliunganisha mpira huo wa chinichini moja kwa moja hadi wavuni.
Nzengeli ambaye amemaliza michuano hiyo akiwa na mabao mawili, pia ndiye aliyeibuka mchezaji bora wa mechi hiyo ya fainali.
Haikuwa rahisi kwa Yanga kupata ushindi kwa namna JKU walivyokuwa imara kwa kushambulia na kudhibiti vyema mashambulizi ya Yanga na haikushangaza dakika 90 za mchezo kwisha kwa bao hilo pekee.
Neva Kabuma wa JKU alianza kulichachafya lango la Yanga dakika ya 36 baada ya kuizidi ujanja safu ya ulinzi ya Yanga akitokea upande wa kushoto wa JKU na kupiga krosi ambayo ilikosa mmaliziaji.
Yanga walijibu shambulizi hilo muda mfupi baadaye lakini Farid Mussa alishindwa kuipatia timu yake bao akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga.
Zikiwa zimesalia dakika tatu timu kwenda mapumziko, Kabuma tena alimzidi kasi beki wa Yanga, Kibwana Shomari na kupiga krosi lakini Dickson Job aliuwahi mpira na kuutoa ikawa kona ambayo haikuzaa matunda.
Dakika ya 59 Yanga walifanya shambulizi jingine baada ya Stephane Aziz Ki kumpenyezea pasi ya chinichini Nzengeli ambaye akiwa amezungukwa na mabeki wa JKU alipisga shuti lililopaa juu ya lango.
JKU nao walifanya shambulizi jingine katika dakika ya 69 baada ya Rashid Ally kuumiliki vyema mpira kabla ya kuukokota kidogo akiwa mbali kidogo na eneo la 18 kabla ya kufumua shuti la mguu wa kushoto ambalo kama si umahiri wa kipa Djigui Diarra mambo yangekuwa mengine.
Kwa ushindi huo Yanga sasa wanakuwa wameweka rekodi ya kulibeba Kombe la Muungano kwa mara ya saba wakiwazidi mahasimu wao Simba ambao wamelibeba mara sita.
Kimataifa Yanga yabeba Kombe la Muungano
Yanga yabeba Kombe la Muungano
Read also