Liverpool, England
Kocha wa Liverpool, Arne Slot amempongeza mtangulizi wake, Jurgen Klopp muda mfupi baada ya timu hiyo kushinda taji la Ligi Kuu England (EPL) jana Jumapili, Aprili 27, 2025.
Liverpool imetwaa taji hilo baada ya kuilaza Tottenham Hotspur mabao 5-1 katika mechi iliyopigwa jana jioni kwenye dimba la Anfield na kumfanya Slot awe kocha wa kwanza kutoka Uholanzi kubeba taji la EPL.
Slot, 46, mara baada ya ushindi huo alisema jambo lililotokea ni kubwa na hadhani kama ana mengi ya kusema badala yake alitumia muda huo kumshukuru mtangulizi wake, Jurgen Klopp
Mara tu baada ya ushindi huo, Slot alianzisha wimbo maarufu ambao Klopp aliwataka mashabiki wa Liverpool wauimbe wakati wa mechi yake ya mwisho mwezi Mei mwaka jana lakini mashairi ya wimbo huo yakabadilishwa kwenye jina la Arne Slot na Jurgen Klopp.
“Nina hakika asilimia 99.9 kama nitaifungua simu yangu lazima kutakuwa na ujumbe kutoka kwa Jurgen, tumekuwa na mawasiliano kwa kipindi kirefu cha msimu, nafikiri alionesha mwisho wa msimu jinsi alivyo na ubinadamu pale aliponitambulisha,” alisema Slot.
Slot aliongeza kwa kusema kwamba jambo la muhimu ni timu aliyoiacha Klopp yenye uwezo wa kubeba taji, utamaduni, uwajibikaji na viwango vya wachezaji kuwa ni mambo ya kipekee.
Liverpool ilibeba taji la EPL mara ya mwisho miaka mitano iliyopita lakini ushindi huo haukuwa na shamrashamra za mashabiki kutokana na janga la Covid 19.
Naye mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah alisema ni jambo la kipekee kwao kubeba taji kwenye dimba la Anfield mbele ya mashabiki wao, tukio ambalo mara ya mwisho lilitokea mwaka 1990.
“Ni jambo la kipekee kubeba taji Anfield, ni ngumu kuelezea, ni tofauti kabisa na mambo yalivyokuwa kabla (mwaka 2020) hali ilivyo sasa haielezeki, wakati ule kulikuwa na maradhi lakini hali ya sasa ni tofauti kwa asilimia 100,” alisema Salah.
Naye beki Virgil van Dijk, nahodha wa kwanza anayetoka nje ya Uingereza kuiongoza Liverpool hadi kubeba taji aliutoa ushindi huo kama zawadi kwa mashabiki duniani kote huku akiitaja Liverpool kuwa ndiyo klabu nzuri zaidi duniani.
Kwa kiungo Alexis Mac Allister taji hilo la EPL yeye alilifurahia kwa namna tofauti akisema limemzidishia furaha baada ya kubeba Kombe la Dunia mwaka 2022 akiwa na timu yake ya taifa ya Argentina.
‘Kushinda Kombe la Dunia na sasa ligi kuu hakika ni jambo la kipekee, lakini pia isingewezekana bila ya wachezaji wenzangu, mimi ni sehemu tu ya jambo hili, hii timu imekuwa bora hasa katika kipindi cha miaka miwili,” alisema Mac Allister.