Barcelona, Hispania
Beki wa zamani wa Barcelona na timu ya taifa ya Brazil, Dani Alves amefutiwa kesi ya kubaka katika mahakama ya rufaa nchini Hispania.
Katika uamuzi huo uliofikiwa Ijumaa hii, mahakama hiyo ya Catalonia imedai kwamba kesi ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 41, ni yenye mashaka na mambo yenye utata.
Februari mwaka jana Alves alihukumiwa kifungo cha jela miaka minne na nusu baada ya kukutwa na hatia ya kumdhalilisha kijinsia mwanamke mmoja tukio alilodaiwa kulifanya mwaka 2022 katika klabu moja ya usiku mjini Barcelona.
Alves ambaye wakati akicheza soka la ushindani aliichezea timu ya taifa ya Brazil mara 126 aliachiwa kwa dhamana Machi mwaka jana wakati rufaa yake ikisikilizwa.
Katika uamuzi wa kumfutia mashitaka mchezaji huyo mahakama ya rufaa ilieleza kuwa hukumu ya awali katika kesi hiyo ilikuwa na mapungufu, haikuwa na ukweli, utata na yenye mashaka kuhusu tukio zima na matokeo yake.
Mahakama ilifafanua kuwa hoja za mlalamikaji zilitakiwa zichunguzwe kwa kina lakini hazikuwa na ushahidi wa ‘fingerprint’ na ushahidi wa kibaiolojia ambao ungeweza kuzipa nguvu.
Sambamba na hilo mahakama ilifafanua kuwa hoja ya mlalamikaji kwamba alilazimika kwenda bafuni na Alves kwa hofu kwamba marafiki wa Alves wangeweza kumfuata hazina mashiko.
Zaidi ya hilo mahakama hiyo pia ilifafanua kwamba kilichoonekana ni kwamba mlalamikaji aliamua kwa hiyari yake kwenda bafuni kwa lengo la kuwa karibu na mshtakiwa ili kupata nafasi ya kwenda ‘kujirusha naye’.
Mahakama pia ilimfutia Alves zuio alilowekewa likiwamo la kusafiri na makatazo mengine ingawa uamuzi huo bado unaweza kukatiwa rufaa katika mahakama ya juu zaidi.
Wakati wote wa sakata hilo, Alves ambaye ilidaiwa siku aliyodaiwa kufanya tukio hilo alikuwa amelewa, amekuwa akisisitiza kwamba hajafanya kosa lolote na kama kuna jambo alilomfanyia mlalamikaji basi ilikuwa kwa makubaliano.
Kimataifa Dani Alves afutiwa kesi ya kubaka
Dani Alves afutiwa kesi ya kubaka
Read also