London, England
Nyota wa Arsenal, Bukayo Saka amefanyiwa upasuaji baada ya kupata majeraha ya misuli na kwa mujibu wa kocha, Mikel Arteta huenda mchezaji huyo akawa nje ya uwanja kwa takriban miezi mitatu.
Arteta alithibitisa hilo hivi karibuni na kufafanua kwamba Saka aliumia misuli ya mguu wa kulia wakati wa mechi dhidi ya Crystal Palace, mechi ambayo Arsenal ilishinda 5-1.
Kocha huyo alifafanua kwamba Saka alifuata taratibu za kawaida kimatibabu na kila kitu kilikwenda vizuri lakini akakikiri kwamba kwa bahati mbaya mchezaji huyo atakuwa nje ya uwanja kwa wiki nyingi tu.
Alipotakiwa kufafanua zaidi muda ambao Saka anatarajia kurudi dimbani Arteta alionekana hana uhakika badala yake alishikilia msimamo wake kwamba ni baada ya wiki nyingi.
“Nafikiri itakuwa zaidi ya miezi miwili, sijui kwa uhakika itachukua muda gani hasa, itategemea alipoumia na jinsi atakavyoanza kupona, wiki ya kwanza au zaidi, ngoja tuone ni vigumu kusema,” alisema Arteta.
Saka ni mmoja wa wachezaji tegemeo kwenye kikosi cha Arsenal hivyo kuumia kwake huenda kukaathiri mbio za timu hiyo katika kulisaka taji la Ligi Kuu England (EPL) msimu huu wa 2024-25.
Arsenal kwa sasa inashika nafasi ya pili kwenye ligi hiyo nyuma ya vinara Liverpool kwa tofauti ya pointi sita wakati Man City ambao ni washindani wengine wa taji hilo kwa miaka kadhaa sasa, hali yao msimu huu si nzuri.