Na mwandishi wetu
Yanga imeanza kurejea katika ubora wake na kuondokana na mikosi ya vipigo vitatu mfululizo baada ya kuichapa Namungo FC mabao 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyopigwa Jumamosi hii.
Kabla ya mechi hiyo iliyopigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Majaliwa, Lindi, Yanga ilipoteza mechi tatu mfululizo hali iliyozua taharuki na kusababisha kutimuliwa kwa kocha Miguel Gamondi.
Katika mechi hizo tatu, Yanga ilifungwa bao 1-0 na Azam FC na baada ya hapo, ikafungwa mabao 3-1 na Tabora United kabla ya kuchukua uamuzi wa kumtimua Gamondi.
Baada ya hapo ikiwa na kocha mpya, mambo yaliendelea kuwa mabaya kwa timu hiyo ilipojikuta ikipoteza kwa mabao 2-0 mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal ya Sudan.
Ushindi wa Namungo umesaidia kupoza machungu waliyokuwa nayo mashabiki wa Yanga ambao baadhi walianza kupoteza matumaini na timu yao wakiamini kasi ya ushindi imefika mwisho na wengine kupoteza matumaini ya timu hiyo kulitetea taji la Ligi Kuu NBC.
Yanga ilianza kuhesabu bao lake la kwanza dakika tano baada ya kuanza kwa kipindi cha pili mfungaji akiwa ni nyota wa kimataifa wa Zambia, Kennedy Musonda.
Idadi ya mabao ya Yanga ilihitimishwa na kiungo wa timu hiyo kutoka nchini Ivory Coast, Pacome Zouzoua aliyefunga bao la pili katika dakika ya 66.
Ushindi wa Yanga umekuja wakati timu hiyo ikicheza bila ya kiungo na nahodha wa timu ya taifa ya Uganda, ‘Uganda Cranes’ Khalid Aucho ambaye alipata majeraha wakati akiiwakilisha timu yake ya taifa.
Aucho amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa wachezaji muhimu kwenye kikosi cha Yanga na baadhi ya wachambuzi wamekuwa wakihusisha matokeo mabaya ya timu hiyo na kukosekana kwa mchezaji huyo.
Soka Yanga yafuta mikosi
Yanga yafuta mikosi
Read also