Na mwandishi wetu
Yanga imetoka kifua mbele dhidi ya mahasimu wao Simba baada ya kuwatandika bao 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyopigwa leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Bao hilo pekee la Yanga lilitokana na makosa ya nyota wa Simba, Kelvin Kijili ambaye alijifunga wakati akiokoa mpira uliotokana na mpira wa adhabu uliopigwa na Clatous Chota Chama.
Chama baada ya kupiga mpira wa adhabu, kipa wa Smba Musa Camara aliufuata na kuuokoa na kurudi uwanjani ndipo ulipomkuta Maxi Nzengeli ambaye shuti lake lililokuwa likielekea kuwa goli liliokolewa na Shomari Kapombe na mpira huo kumgonga Kijili kabla ya kujaa wavuni.
Kwa ushindi huo Yanga sasa imefikisha pointi 15 katika ligi hiyo ikiwa imecheza mechi tano na haijapoteza hata mechi moja huku ikishika nafasi ya pili nyuma ya Singida Black Stars inayoshika usukani ikiwa na pointi 16.
Simba inashika nafasi ya nne nyuma ya Azam FC ikiwa na pointi 13 katika mechi sita, imepoteza mechi moja ambayo ni ya leo dhidi ya mahasimu wao Yanga na sare moja dhidi ya Coastal Union.
Simba ndio waliouanza mchezo wa leo kwa kasi na katika dakika tano za awali walilisumbua lango la Yanga na kusababisha mpira wa adhabu iliyopigwa na Jean Ahoua na kuzaa kona ambayo haikuzaa matunda.
Dakika ya saba Ateba aliunasa mpira na kujaribu kumchenga kipa wa Yanga, Djigui Diara ambaye aliuokoa mpira miguuni mwa mchezaji huyo kabla ya kumkuta Mutale ambaye shuti lake liliwainua vitini mashabiki wa Simba lakini Diarra akaonesha umahiri kwa mara nyingine.
Yanga walijibu mapigo dakika ya 21 baada ya Pacome Zouzoua kupiga krosi ambayo ilimpita kipa wa Simba na kumkuta Nzengeli ambaye alipiga shuti lisilo na macho ambalo lilitoka nje ya lango.
Pacome kwa mara nyingine dakika ya 42 aliuwahi mpira uliokuwa ukitoka nje kwenye lango la Simba na kuurudisha uwanjani na kutoa pasi iliyomkuta Stephane Aziz Ki.
Aziz Ki akiwa katika nafasi nzuri alipiga shuti ambalo liliokolewa na kipa wa Simba kabla ya kugonga mwamba na kuokolewa kwa mara nyingine na kipa huyo.
Katika mechi hiyo makocha Fadlu Davids wa Simba na Miguel Gamondi wa Yanga walifanya mabadiliko kadhaa lakini mwisho wa siku ni Yanga walioneemeka na mabadiliko hayo.
Soka Yanga yaitandika Simba 1-0
Yanga yaitandika Simba 1-0
Related posts
Read also