Berlin, Ujerumani
Nani kubeba taji la Euro 2024, ni kitendawili kilichotatiza mashabiki wa soka kwa siku kadhaa lakini Jumapili hii kimeteguliwa kwa Hispania kubeba taji hilo baada ya kuilaza England mabao 2-1.
Ushindi wa Hispania unaendeleza maumivu makali ya England ambayo ilikuwa na matumaini ya kubeba taji hilo na hivyo kufuta unyonge wa taifa hilo wa miaka 58 bila taji lolote kubwa la soka.
Mechi iliyozikutanisha timu ambazo awali hazikupewa nafasi ya kufika mbali lakini zilivuka hatua moja hadi nyingine na kukutana katika fainaili iliyopigwa mjini Berlin kwenye dimba la Olimpiki.
Aliyepeleka msiba England alikuwa ni Mikel Oyarzabal ambaye alifunga bao la ushindi dakika ya 86 akiunganisha krosi ya Marc Cucurella na Hispania kulilinda bao hilo hadi mwamuzi anapuliza filimbi ya kumaliza mchezo.
Kocha wa England, Gareth Southgate na wachezaji wake hawakuamini kilichotokea baada ya filimbi ya kumaliza mchezo kupulizwa, wakabaki vichwa chini kama watu wasiojua hatma yao baada ya matokeo hayo.
Hispaniam vinara wa taji hilo 2012, walianza kuzichana nyavu za England dakika mbili baada ya kuanza kipindi cha pili kwa bao la Nico Williams aliyeitumia pasi ya Lamine Yamal kufumua shuti lililomshinda kipa wa England, Jordan Pickford.
England walipambana na dakika 25 baadaye walisawazisha bao hilo kupitia Cole Palmer ambaye aliitumia pasi ya Jude Bellingham na hivyo kuibua matumaini mapya kwa mashabiki wa England ambao waliwazidi kila kitu wenzao wa Hispania.
Baada ya bao la kusawazisha kukawa na kila dalili hasa nje ya uwanja kwa mashabiki kwamba huu ulikuwa mwaka wa England hasa baada ya kupindua meza katika mechi zilizopita dhidi ya Slovakia, Switzerland na Uholanzi.

Katika mechi hizo England ilionesha kila dalili za kushindwa lakini ilifanikiwa kubadili matokeo na kusonga mbele hadi kufikia hatua ya fainali, imani iliendelea kuwa hivyo kwa mashabiki wa timu hiyo kabla ya kutulizwa na bao la Oyarzabal.
Maumivu ya England ambayo yamekuja baada ya kuwapo matumaini makubwa yanabadili mambo mengi kuhusu mambo ya baadaye ya timu hiyo moja kati ya hayo ni kuhusu kocha Southgate na nahodha wake Harry Kane.
Kane ameshindwa kuonesha ubora ambao amekuwa nao katika kikosi cha Bayern Munich na hata katika mechi ya fainali alilazimika kutupwa benchi na hoja inayoibuka sasa ni je ataendelea kuwa nahodha wa timu hiyo.
Kuhusu Southgate, hatma yake muda mrefu sasa imekuwa mjadala lakni baada ya timu hiyo kufikia hatua ya fainali kulikuwa na hoja ya kumtaka aendelee kikonoa kikosi hicho hadi kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026, je msimamo huo bado upo vile vile?