Munich, Ujerumani
Winga wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo amethibitisha kuwa fainali za soka Euro 2024 ni za mwisho kwake akiwa na timu yake ya taifa na hakuna ubishi kwamba zitakuwa zenye kuvutia.
Hii ni mara ya sita kwa Ronaldo kushiriki fainali hizo maarufu Euro ambazo hufanyika kila baada ya miaka minne zikishirikisha timu za mataifa ya Ulaya.
Fainali zijazo za Euro yaani Euro 2028 zitafanyika Uingereza na Jamhuri ya Ireland na wakati huo, Ronaldo, nyota wa zamani wa timu za Man United, Real Madrid na Juventus atakuwa na miaka 43.
“Hakuna ubishi kwamba hizi ni fainali za mwisho kwangu za Euro, lakini si kwamba ninazungumza kwa sababu ya hamasa tu, hapana ni masuala ya soka na mapenzi yangu kwa kila kitu kwenye mchezo huu,” alisema.
“Mvuto nilionao katika mchezo huu, namna ninavyoupenda, nawaona mashabiki, familia yangu na watu waliojaa mapenzi ya soka, hivyo si suala la kutengana na soka moja kwa moja, kwani ni nini kingine kwangu ninachoweza kukifanya ili nishinde?” alihoji Ronaldo.
Ronaldo ambaye alianza kuichezea timu ya taifa ya Ureno mara ya kwanza mwaka 2003, aliisaidia kubeba taji la michuano hiyo mwaka 2016 na ndiye kinara wa mabao kwa sasa akiwa ameifungia timu hiyo mabao 130.
“Jambo muhimu zaidi katika safari hii ni ule mvuto ambao bado ninao wa kuendelea kuwa hapa, ni miaka 20 ya kuiwakilisha na kuichezea timu ya taifa, kuwapa watu, familia yangu na watoto wangu furaha, hilo ndilo linalonihamasisha zaidi,” alisema Ronaldo.
Juzi Jumatatu Ronaldo alikuwa katika majaribu baada ya mkwaju wa penalti alioupiga kuokolewa na kipa wa Slovenia Jan Oblak katika dakika ya 114 ingawa Ureno walishinda katika penalti tano tano na kufuzu kucheza robo fainali.

Baada ya kukosa penalti hiyo, Ronaldo ambaye kwa sasa anaichezea klabu ya Al Nassr ya Saudi Arabia alijikuta akimwaga chozi kabla ya kutulizwa na wachezaji wenzake.
“Ni mambo ya soka, wale ambao hushindwa ndio hao hao ambao hujaribu, wakati wote nitakuwa mwenye kufanya katika ubora wangu niwapo na jezi hii, bila kujali iwe ni kushindwa au kushinda,” alisema Ronaldo.