Nigeria yaichapa Sao Tome 10-0
Timu ya Taifa ya Nigeria au Super Eagles imeweka rekodi katika mbio za kuwania kufuzu Afcon 2023 baada ya kuichapa nchi yenye watu wasiozidi 250,000 ya Sao Tome kwa mabao 10-0.
Ushindi huo uliopatikana jana usiku unawafanya Nigeria waliokuwa ugenini katika mechi hiyo kuongoza Kundi A wakiwa na pointi sita na mabao 12 ya kufunga baada ya ushindi wa mabao 2-1 walioupata katika mechi yao ya kwanza dhidi ya Sierra Leone.
Karamu ya mabao ya Super Eagles ilianzia dakika ya tisa kwa bao la kichwa lililofungwa na Osimhen ambaye aliitumia krosi ya Moses Simon, dakika ya 28 ushirikiano wa wawili hao ulizaa bao la pili safari hii likifungwa na Simon akiitumia pasi ya Osimneh.
Mabao hayo hayakuifanya Sao Tome kuchanganyana badala yake walitulia na kucheza mpira wa kusaka bao huku wakionyesha dalili zote za kutoa ushindani lakini dakika mbili kabla ya mapumziko juhudi zao zilikatishwa tamaa kwa bao la tatu lililofungwa na Moffi ambaye aliituliza vyema krosi iliyotokea upande wa kulia kabla ya kuujaza mpira wavuni.
Dakika tatu baada ya kuanza kipindi cha pili, Nigeria walionyesha jinsi walivyopania kuiadhibu Sao Tome baada ya kuandika bao la nne mfungaji akiwa ni Osimhen tena safari hii akinufaika na krosi safi iliyochongwa na Ademola Lookman.
Dakika saba baadaye, Nigeria waliandika bao la tano lililofungwa na Peter Etebo kwa mpira wa adhabu lakini kabla Sao Tome hawajatulia walifungwa bao sita lililopatikana dakika ya 61 mfungaji akiwa Moffi akiitumia krosi ya Sanusi Zaidu iliyotokea upande wa kushoto.
Kabla Sao Tome hawajatulia, dakika mbili baadaye walichapwa bao la saba mfungaji akiwa ni Lookman akiumalizia mpira uliopigwa na Moffi na kuookolewa na kipa wa Sao Tome.
Bao la nane la Nigeria lilifungwa na Osimhen tena katika dakika ya 65 kabla ya kuongeza bao la tisa katika dakika ya 84 na hivyo kuwa bao lake la nne katika mechi hiyo, safari hii shuti lake likimpita kipa wa Sao Tome katikati ya miguu yake.
Emmanuel Dennis aliyeingia akitokea benchi alikamilisha karamu ya mabao kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa dakika chache kabla ya mpira kumalizika baada ya mfungaji kuchezewa rafu katika eneo la penalti.
Katika mechi nyingine za jana za Afcon 2923 matokeo yalikuwa kama ifuatavyo
Liberia 0-2 Morocco
Sierra Leone 2-2 Guinea Bissau