Na mwandishi wetu
Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Patrice Motsepe amesema bao la kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephanie Aziz Ki dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini lilikuwa halali.
Motsepe amezungumza hayo leo Ijumaa na waandishi wa habari mara baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Zanzibar alipokwenda kuhudhuria fainali za African Schools Football Championship (ASFC) 2024.
“Ngoja niwaambie kitu, nikiwa kama Rais wa Caf ninaipenda klabu iliyopo Africa na nilisema kitu kwa Rais Wallace (Karia, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), tulipokutana baada ya mechi ya Yanga na Mamelodi nilisema nadhani lile ni goli,” alisema Motsepe aliyewahi kuwa Rais wa Mamelodi.
“Ingawa Rais wa Caf hapaswi kutoa maoni kuhusu maamuzi ya waamuzi lakini kwangu binafsi nilivyorudia kuangalia lilikuwa ni goli halali lakini naheshimu sana taratibu zote za maamuzi na tuna jukumu la kutakiwa kulinda na kuheshimu maamuzi ya waamuzi, VAR, mechi kamishna wa michezo kwa afya ya soka letu,” alifafanua Motsepe.
Bao hilo la Aziz Ki lilizusha utata mkubwa wakati Yanga ikicheza mechi yake ya mkondo wa pili wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi uliopigwa Aprili 5, mwaka huu jijini Pretoria.
Baada ya bao hilo ambalo Aziz aliupiga mpira nje ya 18 na kugonga mwamba wa juu na mpira huo kudunda ndani ya mstari wa goli kabla ya kurejea uwanjani, mwamuzi Beida Dahane kutoka nchini Mauritania alikubaliana na maamuzi ya waamuzi wa chumba cha VAR kuwa si bao ambapo mashabiki wengi waliona hayakuwa maamuzi sahihi.
Motsepe pia ameendelea kuzipongeza klabu za Simba na Yanga kwa kuendelea kuonesha mfano mzuri wa mashabiki wanaoenda kuujaza uwanja kwa kusapoti timu zao zinapocheza.