Munich, Ujerumani
Kocha wa Bayern Munich, Thomas Tuchel amethibitisha kuwa ataachana na timu hiyo mara baada ya msimu huu licha ya kuwapo mazungumzo kuhusu uwezekano wa kuendelea na kibarua hicho.
Bayern ilitangaza Februari mwaka huu kwamba imekubliana na Tuchel mwenye umri wa miaka 50 kuwa ataachana na timu hiyo akiwa amebakisha mwaka mmoja katika mkataba wake.
Tuchel amepitia katika msimu mgumu na timu hiyo ambayo imepoteza taji la Ligi Kuu Ujerumani au Bundesliga mbele ya Bayer Leverkusen baada ya kulibeba kwa miaka 11 mfululizo.
Baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo walisikika hivi karibuni wakiendesha kampeni kumtaka kocha huyo wa zamani wa Chelsea kuendelea kuinoa timu hiyo lakini Tuchel amesema kwamba hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa katika suala hilo.
“Makubaliano yetu ya tangu Februari yanabaki kama yalivyo,” alisema Tuchel ambaye alikabidhiwa majukumu ya kuinoa timu hiyo, Machi 2023.
Habari za Tuchel kubaki Bayern zilipata nguvu baada ya kocha huyo kuiwezesha timu hiyo kuitoa Arsenal katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini ilijikuta ikishindwa kutamba mbele ya Real Madrid katika nusu fainali ya ligi hiyo.
Bayern imekuwa ikihaha kusaka mrithi wa Tuchel ambaye katika siku za karibuni zimekuwapo habari kwamba huenda akajiunga na Man United kuchukua nafasi ya Erik ten Hag.
Makocha waliotajwa kuwindwa na Bayern, Xabi Alonso wa Leverkusen na Ralf Rangnick wa timu ya taifa ya Austria wote wameikataa ofa hiyo.
Alonso alikataa ofa hiyo akidai kwamba anaamini bado anahitaji kumalizia kazi aliyoianza akiwa na Leverkusen wakati Rangnick naye alisema anataka kuendelea na kibarua chake Austria.
Kimataifa Tuchel atangaza, anaondoka Bayern
Tuchel atangaza, anaondoka Bayern
Read also