Na mwandishi wetu
Klabu ya Simba imeelezwa kuwa inatarajia kuachana na nyota wake tisa mwishoni mwa msimu huu akiwemo kipa mmoja, mabeki wawili, viungo wawili, mawinga wawili na washambuliaji wawili.
Taarifa zilizoifikia Green Sports leo Jumatatu zinafafanua kuwa wachezaji watakaotemwa, wengine baadhi ni wachezaji wa zamani na baadhi ya waliosajiliwa hivi karibuni.
Lengo la uamuzi huo imeelezwa kuwa ni kwa ajili ya kupisha wengine kusajiliwa ili kuboresha timu hiyo kwa msimu ujao wa mashindano.
Mbali na hilo chanzo kutoka kwa Wekundu hao kimesema pia kuhusu kocha mpya anayekuja kuchukua nafasi ya Abdelhak Benchikha, uongozi upo katika mchakato mzito huku baadhi ya majina yakiendelea kujadiliwa.
“Ukiachana na jina la kocha wa Al Hilal, Florent Ibenge ambalo limekuwa likijadiliwa hivi karibuni licha ya kuwepo kwa majina mengine lakini kama unavyosikia kuhusu Ibenge. Kwenye suala la usajili pia watatemwa takriban tisa, hata suala la Kibu (Dennis) uongozi unafahamu ushawishi kutoka kwa klabu fulani ambao wanataka kumsajili.
“Kwa sasa ofa rasmi ya klabu inawasilishwa, kuna mkutano na nyota huyo pamoja na viongozi umepangwa wiki ijayo kuongelea mustakabali wake lakini ni kuangalia na wachezaji wengine ambao mikataba yao imefikia tamati na kuongezwa,” kilieleza chanzo hicho kwa sharti la kutotajwa jina lake.
Kuhusu Kibu, hivi karibuni amekuwa akitajwa mno kuwaniwa na wapinzani wa Simba, Yanga ambao hawajatoka hadharani kufafanua hilo ingawa inaelezwa ni mpango wa kocha wa Yanga, Miguel Gamondi.
Hata hivyo meneja wa habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alinukuliwa hivi karibuni akizungumzia taarifa za usajili ambapo alisema wanachokifanya sasa ni kubaki na wale bora wenye moyo wa kuitumikia klabu hiyo.