Na mwandishi wetu
Serikali kupitia Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo ina mpango wa kuunda timu tatu imara za soka za taifa kulingana na umri ambazo zitashiriki fainali za Afcon 2027 na michuano mengine ambayo nchi itashiriki.
Naibu Waziri wa wizara hiyo, Hamisi Mwinjuma ‘MwanaFA’ amesema hayo Jumatatu hii wakati akijibu maswali ya nyongeza ya Mbunge wa Jimbo la Magomeni, Mwanakhamisi Kassim Said (CCM).
Mbunge huyo alitaka kujua mkakati wa Serikali kuandaa timu ya Taifa ili ishindane kwenye michuano ya Afcon.
Katika ufafanuzi wake, Waziri Mwinjuma alisema Serikali imeandaa mkakati wa kuandaa timu si tu kwa ajili ya Afcon 2027, bali kwa mashindano mengine ambayo Tanzania itashiriki na zitagharamiwa na Serikali kwa asilimia 100.
Alisema miongoni mwa mkakati huo ni kutengeneza timu tatu za Taifa zitakazopishana umri. Ya kwanza itakuwa ni ya vijana chini ya miaka 17, itakayotokana na wanafunzi kupitia michezo ya Umiseta ya kila mwaka inayoshirikisha shule za sekondari.
“Tukishawapata wachezaji hawa tutawaweka kwenye shule moja ambayo tumeshaiteua na watasimamiwa na walimu magwiji. Itapata mechi za mazoezi ya kutosha za ndani na nje. Kila mwaka wachezaji hao tutakuwa tunawapeleka kwenye akademi zenye mafanikio nje ya nchi ili kuendeleza vipaji tayari kulitumikia Taifa,” alisema.
Alisema timu ya pili itakuwa inaundwa na vijana wa umri wa chini ya miaka 23 ambao wanacheza ligi mbalimbali ndani na nje ya nchi na watakuwa wakikutana wakati wakiwa kwenye mapumziko ya timu zao.
Alisema pia ili kuhakikisha timu ya Taifa inafanya vizuri katika mashindano hayo, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo ujenzi wa viwanja vya mpira katika majiji ya Dodoma na Arusha pia utafanyika ukarabati wa Viwanja vya Benjamin Mkapa na Uhuru vilivyopo Dar es Salaam.
Sambamba na hilo, serikali pia itakuwa ikiwatafuta na kuwaleta nchini wachezaji wenye asili ya Tanzania wanaoishi na kucheza nje ya nchi ili kuchezea timu ya Taifa.