Na mwandishi wetu
Baada ya sare tasa dhidi ya JKT, Yanga imeendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu NBC baada ya kuichapa Coastal Union bao 1-0 katika mechi iliyopigwa Jumamosi hii jioni.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye dimba la Azam Complex, bao hilo pekee lililoihakikishia Yanga pointi tatu lilifungwa na Joseph Guede dakika ya 75 akimalizia pasi ya Kennedy Musonda.
Dakika tano kabla ya kuingia kwa bao hilo, mambo yalianza kuwaharibikia Coastal walipolazimika kubaki wachezaji 10 uwanjani baada ya mwamuzi kumpa kadi nyekundu beki wa timu hiyo, Lameck Lawi.
Lawi alijikuta akipewa kadi hiyo baada ya kumvuta jezi kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephanie Aziz Ki ambaye alikuwa anaelekea kuipatia Yanga bao.
Kwa ushindi huo Yanga inaendelea kushikilia usukani wa ligi hiyo ikiwa imefikisha pointi 62 katika mechi 24 wakati Coastal Union inabaki katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 33 nayo hadi sasa ikiwa imecheza mechi 24.
Azam inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 54 katika mechi 24 wakati mahasimu wa Yanga, Simba wao wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 46 katika mechi 21.
Soka Yanga yainyuka Coastal 1-0
Yanga yainyuka Coastal 1-0
Read also