Manchester, England
Klabu ya Manchester United imeweka wazi kuwa haina mpango wa kubadili maamuzi ya awali ya kuachana na kiungo wake mkongwe, Casemiro mwishoni mwa msimu huu.
Casemiro mwenye umri wa miaka 34, Januari mwaka huu alitangaza kuwa ataachana na klabu hiyo baada ya mkataba wake wa sasa unaompatia mshahara wa Pauni 350,000 kwa wiki utakapofikia ukingoni.
Baada ya Casemiro kutoa kauli hiyo kumekuwa na mtazamo tofauti kutokana na kiwango cha mchezaji huyu kuvutia wengi kiasi cha kuibua uvumi kwamba huenda akaongezewa mkataba lakini klabu yake imelikana hilo.
Kutokana na kuibuka mtazamo huo, Man United imeweka wazi kuwa haitokuwa tayari kumpa mkataba mpya kiungo huyo wa zamani wa Real Madrid na kilichopo ni kwamba baada ya msimu huu atakuwa mchezaji huru.
Mmoja wa wamiliki wa klabu hiyo bilionea, Sir Jim Ratcliffe aliwahi kunukuliwa kuhusu Casemiro ambaye mshahara wake kwa mwaka unafikia Pauni 18 milioni ambapo tajiri huyo alielezea mkakati wake wa kupunguza gharama za klabu hiyo.
Habari zinadai kwamba Casemiro mwenyewe ndiye aliyetaka habari kuhusu mkataba wake kuwekwa wazi ili kuepuka kuibuka kauli tata mwishoni mwa msimu ingawa kiwango cha mchezaji huyo kimeibua mtazamo tofauti.
Casemiro ndiye aliyefunga bao la kwanza katika mechi na Aston Villa na baada ya bao hilo alishangilia kwa kuruka juu mbele ya mashabiki na kuibusu jezi ya klabu hiyo zaidi ya mara moja.
Tukio hilo liliwaibua mashabiki ambao walianza kuimba ‘mwaka mmoja zaidi kwa Casemiro’ na kurudia wimbo huo wakati mchezaji huyo akitoka uwanjani baada ya mechi hiyo huku akiibusu jezi zaidi ya mara moja.
Nahodha wa Man United, Bruno Fernandes na beki Leny Yoro nao baada ya mechi walisema wana matumaini Casemiro atabaki katika klabu hiyo ingawa klabu haina mpango wa kubadili uamuzi wa awali wa kuachana na kiungo huyo kutoka Brazil.
Wakati wachezaji wakiwa na mtazamo huo, kocha wa muda wa timu hiyo, Michael Carrick pia amesema kwamba anadhani hakutakuwa na kubadili uamuzi kuhusu mambo yajayo ya Casemiro na klabu hiyo ya Old Trafford.
“Pindi jambo linapokuwa limefanyiwa maamuzi kidogo inakuwa rahisi na kila mmoja anaelewa mazingira, mchango wake kwenye timu umekuwa wa kipekee, na kumekuwa na tukio zuri baada ya mechi kati yake na mashabiki, atafurahia hilo,” alisema Carrick.
