Barcelona, Hispania
Mwanadada, Rafaela Pimenta ambaye ni wakala wa mshambuliaji wa Man City, Erling Haaland ameipuuza habari inayodai kwamba kumekuwapo na mazungumzo kuhusu mpango wa Haaland kuhamia Barcelona au Barca.
Mmoja wa wagombea nafasi ya urais katika klabu ya Barcelona, Victor Font katika habari hiyo anadaiwa kudai kwamba yamekuwapo mazungumzo ya kumsajili mshambuliaji huyo atakapoihama Man City.
Rafaela hata hivyo alikana kuwapo kwa mazungumzo ya aina yoyote kuhusu mpango huo akisema kwamba hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanyika kuhusu uwezekano wa jambo hilo.
Badala yake mwanadada huyo alifafanua kwamba Haaland aliongeza mkataba na Man City miezi kadhaa liyopita, mkataba ambao utafikia ukomo mwaka 2034 na ana furaha kuwa katika klabu hiyo.
“Kila kitu kinakwenda vizuri, kwa Haaland na hana lolote ambalo amelijadili kuhusu uwezekano wa kuhama, hakuna kitu hicho kwani kila kitu kinamuendea vizuri Man City,” alisisitiza Rafaela.
Kwa upande wake Font awali alinukuliwa akisema kwamba mpango wa kumsajili Haaland haraka hautowezekana lakini kama atachaguliwa kuiongoza Barca katika nafasi ya urais anaamini suala la kumsajili mshambuliaji huyo litawezekana.
Uchaguzi katika klabu ya Barcelona unatarajia kufanyika Jumapili ambapo Font atachuana vikali kwenye sanduku la kura na rais anayemaliza muda wake Joan Laporta.
