Porto, Ureno
Kocha wa Benfica, Jose Mourinho amemshutumu kocha msaidizi wa FC Porto akidai kocha huyo alimuita msaliti mara 50 mara baada ya Mourinho kupewa kadi nyekundu katika mechi baina ya timu hizo.
Mechi hiyo baina ya mahasimu hao wa soka nchini Ureno iliisha kwa sare ya mabao 2-2 huku Benfica ikipambana hadi kusawazisha mabao hayo baada ya kuwa nyuma kwa mabao 2-0.
Mkombozi wa Benfica katika mechi hiyo alikuwa Leandro Barreiro, mchezaji aliyeingia akitokea benchi na kufunga bao la kusawazisha dakika mbili kabla ya mpira kumalizika, bao ambalo lilisababisha kuzuka tafrani.
Katika tafrani hizo, Mourinho alijikuta akipewa kadi nyekundu baada ya kuonekana akiwa katika mzozo na watu wa kwenye benchi la timu ya FC Porto.
Alipoulizwa sababu ya kupewa kadi nyekundu na kutolewa nje, Mourinho alisema hajui ingawa mwamuzi alimwambia kwamba alipewa kadi hiyo kwa kosa la kuwapiga na mpira watu wa kwenye benchi la FC Porto.
“Mwamuzi ameniambia alinipa kadi kwa sababu niliwapiga na mpira watu wa FC Porto jambo ambalo ni uwongo, kwa sababu niliupiga mpira kwa mashabiki,” alisema Mourinho.
Mourinho kocha wa zamani wa timu za Chelsea, Real Madrid, Inter Milan, Tottenham, AS Roma, Man United na FC Porto, alifafanua kwamba huwa ana kawaida ya kufurahia goli kwa kuupiga mpira jukwaani kwa mashabiki kwa lengo la kumpa mpira huo shabiki mwenye bahati.
Kocha huyo mwingi wa vituko ambaye pia anajulikana kwa jina la Speacial One, hata hivyo alisema anajua yeye si mahiri katika mbinu za soka ingawa mpira ule aliupiga lengo lake ni uende jukwaani kwa mashabiki.
Kuhusu kocha msaidizi wa FC Porto, Mourinho alifafanua kuwa kocha huyo alimuita msaliti mara 50 na alimtaka amwambie yeye msaliti kwa lipi wakati kila timu alizokuwa alijitoa kwa moyo wote na maisha yake kwa saa 24.
“Kutukanwa na mashabiki hilo ni jambo jingine lakini kocha mtaalam mwenzangu ananiita mimi msaliti, kwa nini? Ninavyojitoa hapa Benfica? Mimi msaliti kwa lipi?,” alihoji Mourinho.
