Na mwandishi wetu
Klabu ya Simba imeendelea kutoa malalamiko yake kuhusu kuwapo kwa jezi feki zenye nembo ya klabu hiyo zinazoendelea kuuzwa katika maeneo mbalimbali nchini na kuahidi kuendesha oeperesheni maalum.
Taarifa ya klabu ya Simba iliyotolewa Jumamosi Machi 7, 2026 imeeleza kuwa uongozi wa klabu hiyo kwa kushirikiana na mzabuni wa jezi, Kampuni ya Jayrutty Investment imebaini kuwapo kwa jezi hizo sokoni.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyoandaliwa na uongozi wa Simba na Jayrutty, jezi hizo ni zile ambazo zilitumiwa kwa ajili ya maandalizi ya msimu yaani pre season.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa jezi hizo hazikuandaliwa kwa ajili ya mashabiki bali ni wachezaji pekee kwa ajili ya kipindi cha pre season.
Uongozi wa Simba na Jayrutty wamebainisha kuwa hakuinufaishi timu wala mzabuni badala yake wanaonufaika ni wezi kwani kitendo hicho ni uhujumu uchumi si kwa klabu tu bali hata nchi.
Katika kukabiliana na tatizo klabu kupitia taarifa hiyo imeahidi kuendesha operesheni maalum ya kukamata jezi feki itakayoanza Jumatatu ya Machi 9, 2026.
“Kuanzia sasa yeyote atakayekutwa anatengeneza, kuuza au kununua jezi hizo atakamatwa na kuchukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Hii si taarifa ya kwanza kwa Simba na Jayrutty kulalamikia kuwapo kwa jezi feki, Desemba mwaka jana, Simba kupitia msemaji wa klabu hiyo, Ahmed Ally walitoa taarifa ya punguzo la bei ya jezi sambamba na kutoa tahadhari ya kuwapo kwa jezi feki katika mikoa kadhaa nchini.
