Riyadh, Saudi Arabua
Nahodha wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo amelazimika kwenda Madrid, Hispania kwa ajili ya matibabu ya misuli baada ya hali kuwa mbaya tofauti na ilivyodhaniwa awali.
Ronaldo, 41, ambaye kwa sasa anaichezea klabu ya Al Nassr ya Saudi Arabia akiwa ameifungia mabao 21 katika mechi 22 za msimu huu, alilazimika kufanyiwa mabadiliko katika mechi ya Jumamosi Machi, 6, 2026 dhidi ya Al Fahya, mechi ambayo Al Nassr ilipata ushindi wa mabao 3-1.
Akizungumzia tukio hilo, kocha wa Al Nassr, Jorge Jesus alisema kwamba Ronaldo anakwenda Madrid ambapo atapatiwa matibabu na mtaalam wake binafsi wa viungo na baada ya hapo atapata muda wa kupumzika.
Haijaweza kufahamika haraka kama mchezaji huyo mwenye rekodi ya kushinda tuzo za Ballon d’Or mara tano atapona haraka na kuiwakilisha Ureno katika mechi za kirafiki dhidi ya Mexico hapo Machi 29 mwaka huu na nyingine dhidi ya Marekani itakayochezwa Aprili Mosi.
“Katika mechi yake ya mwisho Cristiano alitoka uwanjani akiwa na matatizo ya misuli, baada ya kufanyiwa vipimo ilionekana wazi kuwa tatizo lilikuwa kubwa kuliko tulivyodhani, anahitaji muda apone na arudi haraka kuisaidia timu,” alisema Jorge.
Ronaldo ambaye hadi sasa ana rekodi ya kufunga mabao 965 katika maisha yake ya soka la ushindani, amewahi kusema kwamba hatarajii kustaafu soka hadi atakapofunga mabao 1,000.
Katika siku za karibuni mchezaji huyo alikuwa katika mgomo baridi na kukosa mechi kadhaa sababu ikidaiwa kuwa ni kutokubaliana na masuala kadhaa ya uwekezaji katika klabu ya Al Nassr ingawa baadaye alisitisha mgomo huo.
Ronaldo alijiunga na Al Nassr Desemba 2022 baada ya mkataba wake na Manchester United kufutwa, kwa sasa ndiye mchezaji anayelipwa fedha nyingi zaidi duniani, mshahara wake unafikia Pauni 177 milioni na Juni mwaka jana alisaini mkataba mwingine wa miaka miwili.
