Na mwandishi wetu
Mwamuzi msaidizi namba moja wa mechi ya mahasimu wa soka Yanga na Simba, Kassim Mpanga (pichani) wa Dar es Salaam amefungiwa miezi sita kwa kosa la kushindwa kutafsiri sheria za soka kwa kukataa bao halali la Simba.
Taarifa ya kamati ya usimamizi na uendeshaji wa ligi ya Bodi ya Ligi Kuu iliyopatikana Machi 6, 2026 ilieleza kuwa katika dakika ya 70 ya mchezo huo, mwamuzi huyo alikataa bao hilo kwa kuonesha kuwa kuna mchezaji aliotea wakati haikuwa hivyo.
Bao hilo la Simba lilifungwa na Seleman Mwalim na baadaye wataalam wa kutafsiri sheria za soka baada ya kufanyia tathmini kupitia video wamebainisha kuwa hakukuwa na kosa lolote kabla ya kufungwa bao hilo.
Naye mwamuzi msaidizi namba mbili wa mechi hiyo, Hamdan Said wa Mtwara amefungiwa miezi mitatu pia kwa kushindwa kutafsiri vyema sheria za soka ambapo dakika ya 61 aliashiria mshambuliaji wa Yanga Prince Dube alikuwa ameotea.
Katika kipindi hicho Yanga walifanya shambulizi langoni mwa Simba na kitendo cha mwamuzi huyo kutoa ishara ya kuotea maana yake ni kwamba shambulizi hilo la Yanga lilikwama wakati mchezaji huyo hakuwa katika mazingira ya kuotea.
Adhabu nyingine katika mechi hiyo hiyo pia ilitolewa kwa klabu ya Simba ambayo imetozwa faini ya Sh milioni tano kwa kuingia Uwanja wa New Amaan kwa kutumia mlango usio rasmi.
Simba pia wametozwa faini nyingine ya Sh milioni tano kwa kosa la kukataa kutumia vyumba vya kubadilishia nguo na badala yake kutumia chumba kinachotumiwa kwa ajili ya mikutano na wanadishi wa habari.
Klabu hiyo pia imetakiwa kulipia gharama za matengenezo ya mlango wa kuingia katika chumba cha mikutano na waandishi wa habari baada ya walinzi wake kuvunja mlango huo na kulazimisha kuingia humo badala ya kutumia chumba cha kubadilishia nguo.
Katika tukio jingine la mechi hiyo, klabu za Simba na Yanga kila moja imetozwa faini ya Sh milioni tano kwa kosa la walinzi wao kugombana na kutoleana lugha chafu jambo lililozua taharuki na kuchafua taswira ya mchezo huo wakati klabu ya Simba ikiingia uwanjani.
Soka Refa aliyekataa bao la Simba afungiwa
Refa aliyekataa bao la Simba afungiwa
Read also
