Na mwandishi wetu
Baada ya sare ya bila kufungana, Yanga imeendeleza rekodi ya kutopoteza mechi katika Ligi Kuu NBC kwa kuicharaza Singida Black Stars mabao 3-0 mechi iliyopigwa Alhamisi Machi 5, 2026 kwenye dimba la Airtel mjini Singida.
Ushindi huo ni hatua nyingine muhimu katika mbio za Yanga kulitetea taji la ligi hiyo ikiwa ndiyo timu inayoshika usukani baada ya kukusanya pointi 32 katika mechi 12 ilizocheza hadi sasa.
Yanga imeizidi JKT Tanzania inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti na pointi nne huku mahasimu wao Simba wanaoshika nafasi ya tatu wakiachwa na Yanga kwa tofauti ya pointi nane.
Mashabiki wa Singida wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani walianza kunyamazishwa na Yanga katika dakika ya 39 kwa bao lililofungwa na Prince Dube aliyeitumia vizuri pasi ya Maxi Nzengeli.
Dakika moja kabla ya muda wa mapumziko, Dube alichezewa rafu katika eneo la penalti na Morris Chukwu na mwamuzi kuamuru ipigwe penalti ambayo ilipigwa na Allan Okelo na mpira kujaa wavuni na kuwa bao la pili la Yanga.
Singida walikianza kipindi cha pili kwa moto wakiwa na matumaini ya kusawazisha mabao lakini mambo yaliwaendea ndivyo sivyo dakika ya 56 baada ya Yanga kupata bao la tatu mfungaji akiwa ni Mudathir Yahya aliyeujaza mpira wavuni baada ya kipa wa Singida, Metacha Mnata kuokoa shuti la Dube.
Soka Yanga yaicharaza Singida 3-0
Yanga yaicharaza Singida 3-0
Read also
