Manchester, England
Man City wamepangwa kukabiliana na Real Madrid katika mechi za mtoano (16 bora) ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, kitendo ambacho kidogo kinaonekana kumshangaza kama si kumshtua kocha wa Man City, Pep Guardiola.
Hii inakuwa mara ya tano timu hizo kukutana katika miaka ya karibuni na jambo hilo ndilo linaloonekana kumshangaza Pep ambaye kwa sasa timu yake inapambana vikali kwenye mbio za taji la Ligi Kuu England.
Kwa Pep kitendo cha kupangwa tena na Real Madrid kitamfanya afikishe idadi ya mechi 15 dhidi ya timu hiyo tangu ajiunge na Man City mwaka 2016 baada ya kupitia na kujipatia mafanikio katika klabu ya Barcelona na baadaye Bayern Munich.
Pep alikiri kwamba kwa kiasi fulani jambo hilo linashangaza lakini alielezea kuwa kuna suala la mfumo wa michuano hiyo na kufafanua kwamba kwa kuwa tayari imeshapangwa hakuna namna.

Kocha huyo pia alisema kwamba kauli yake haina maana kwamba timu nyingine hazina changamoto kwa wapinzani wao kwani kuwa na imani hiyo ni kuzidharau timu hizo kwa kuona wao tu (Man City) ndio wenye wapinzani wagumu.
Pep alisema kuwa na imani kwamba wao tu ndio wenye mpinzani mgumu ni dharau ni kama vile kuona mechi kati ya Newcastle na Barcelona au Atlético Madrid na Tottenham ni rahisi wakati kiujumla Ligi ya Mabingwa ni ngumu.
“Pia sisemi Real Madrid si timu ngumu, kila mtu anafahamu ugumu wao, lakini ni hivyo hivyo kwa timu nyingine, unaweza kuzitaja, zote zipo katika hatua ngumu, unapotaka kusonga mbele katika hatua hii kwenye ligi ya mabingwa lazima ushinde dhidi ya timu bora, vinginevyo huna hadhi ya kwenda popote,” alisema Pep.
Nje ya hiyo hiyo ya Pep, kuna vita ya washambuliaji mahiri wa timu hizo mbili, Kylian Mbappe wa Real Madrid na Erling Haaland wa Man City ni yupi ambaye atafunga mabao ya kuisaidia timu yake kusonga mbele.

Mechi za kwanza katika hatua hiyo zitapigwa kati ya Machi 10 na 11 mwaka huu na marudiano Machi 17 na 18, hadi hapo kila timu itakuwa imejua hatma yake kwenye michuano hiyo mikubwa ya klabu Ulaya na duniani.
Timu pinzani 16 bora Ligi ya Mabingwa Ulaya
Paris St-Germain vs Chelsea
Galatasaray vs Liverpool
Real Madrid vs Manchester City
Atalanta vs Bayern Munich
Newcastle United vs Barcelona
Atletico Madrid vs Tottenham
Bodo/Glimt vs Sporting CP
Bayer Leverkusen vs Arsenal
