Na mwandishi wetu
Wakati Yanga ikishangilia ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mechi ya Ligi Kuu NBC, mambo hayakuwa mazuri kwa mtani wake Simba aliyelazimishwa sare ya bila kufungana na Dodoma Jiji FC.
Mechi hizo zilizochezwa Jumatano Febuari 25, 2026 ni mechi za mwisho baina ya watani hao wa jadi kabla ya kukutana Machi Mosi, 2026 kwenye dimba la New Amaan, Zanzibar katika mwendelezo wa mechi za ligi hiyo.
Karamu ya mabao matano ya Yanga au mkono ilipatikana kwenye Uwanja wa KMC, Kinondoni, Dar es Salaam kwa mabingwa hao watetezi wa ligi kuandika bao la kwanza kunako dakika ya saba mfungaji akiwa ni Mohamed Hussein au Zimbwe Junior baada ya kuinasa pasi ya Prince Dube.
JKT walipambana na kuonesha uhai na hadi timu zinakwenda mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa bao hilo pekee licha ya mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa JKT.
Kipindi cha pili mambo yalianza kuwaharibikia JKT katika dakika ya 60 baada ya kufungwa bao la pili, mfungaji akiwa Dilson Depu aliyeitumia vizuri pasi ya Israel Mwenda.
Matumaini ya JKT kutaka bao la kufufua matumaini yalianza kufifia dakika tatu baada baada ya bao la Depu pale, Mudathir Yahya alipoiandikia Yanga bao la tatu.
Mabao mengine mawili ya Yanga yalifungwa na Dube katika dakika ya 83 na Shekhan Khamis aliyekamilisha karamu ya mabao hayo katika dakika ya 89.
Kwa ushindi huo Yanga imejikita kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 28 katika mechi 10 sawa na JKT ingawa Yanga ina faida katika mabao ya kufunga na kufungwa.
Kwa upande wa Simba hali ilikuwa tete kwa dakika zote 90 kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana matokeo yanayowafanya mashabiki wa timu hiyo kubaki wakitafakari hatma ya timu yao kabla ya kuivaa Yanga.
Mechi hiyo kwa upande mwingine ilikuwa neema kwa kipa wa Dodoma Jiji, Daniel Mgore ambaye aliibuka mchezaji bora kwa namna ambavyo alifanikiwa kuzima ndoto za washambuliaji wa Simba kupata bao katika dakika zote 90.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, Azam FC ikiwa nyumbani kwenye dimba la Azam Complex ilitoka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mtibwa Sugar.
Soka Simba yakwama, Yanga yapiga mtu mkono
Simba yakwama, Yanga yapiga mtu mkono
Read also
