Manchester, England
Kocha wa Man United, Michael Carrick amesema hatarajii mgomo wa mashabiki dhidi ya wamiliki wa klabu hiyo, Familia ya Glazer na Sir Jim Ratcliffe kuiathiri timu yake katika mechi dhidi ya Fulham Jumapili hii.
Hali ya utulivu imeanza kurejea katika klabu hiyo ya Old Trafford chini ya Carrick aliyeanza kibarua kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya mahasimu wao wa jiji la Manchster, Man City kisha kuichapa Arsenal mabao 3-2 wiki iliyopita.
Man United inatarajia kuendeleza wimbi la ushindi Jumapili hii Februari mosi, 2026 dhidi ya Fulham wakati huo huo kukiwa na utata kutoka maelfu ya mashabiki ambao inatarajiwa kabla ya mechi hiyo wataanika kero yao ya kuwapinga wamiliki wa klabu hiyo.
Familia ya Glazer ambayo iliinunua klabu hiyo mwaka 2005 imekuwa ikisakamwa na mashabiki kama ambavyo imekuwa kwa Sir Jim Ratcliffe ambaye alinunua sehemu ya hisa za klabu hiyo mapema mwaka 2024 naye amejikuta katika hali hiyo hasa katika miezi ya karibuni.
“Sidhani kama kuna uhusiano wowote wa hali hiyo na ushindi wa mechi mbili, niwe mkweli nadhani haina athari yoyote kwa timu, nawaheshimu mashabiki, ni watu wa kipekee, wamekuwa na timu hii kwa muda mrefu,” alisema Carrick ambaye alikabidhiwa timu hiyo Januari 8 mwaka huu baada ya kutimuliwa kwa Ruben Amorim.
Carrick ambaye aliwahi kuwa mchezaji wa nafasi ya kiungo katika timu hiyo alisema mashabiki wana mambo yao mazuri na mabaya pia lakini hawamsemi yeye kwa ubaya na wachezaji pia hawana ubaya nao.
Alisema uhusiano wake na mashabiki katika wiki chache zilizopita umekuwa ni wa kipekee na kusisitiza kwamba mashabiki wamekuwa hivyo kwa wakati wote na anaamini wataendelea kuwa hivyo.
